Habari Mseto

Maswali yaibuka kufuatia kifo cha daktari Mkenya nchini Cuba

March 20th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na WINNIE ATIENO

MASWALI mengi yameibuka kufuatia kifo tatanishi cha daktari Mkenya aliyeenda nchini Cuba na wenzake kusoma, kufuatia makubaiano kati ya serikali ya Kenya na Cuba.

Daktari huyo kutoka wilayani Likoni kaunti ya Mombasa, anadaiwa kujiua kufuatia mzongo wa maisha ya Cuba na changamoto alizokuwa akipitia.

Familia ya marehemu ikiongozwa na dadake ambaye ni Mbunge wa Likoni Mishi Mboko, alisema wanaendelea na mipango ya kung’amua kifo cha nduguye mdogo.

Hata hivyo, aliwahakikishia wakenya kuwa upasuaji ambao unatarajiwa kufanywa nchini humo utabainisha kiini cha kifo Dkt Hamisi Ali Juma.

Hata hivyo, chama cha madaktari nchini kimeitaka serikali kusitisha mpango wa masomo kati ya Kenya na Cuba ikisisitiza haijawasaidia madaktari wa humu nchini.

Badala yake, chama hicho kimeisihi serikali kuwapeleka madaktari hao kusomea vyuo vikuu vitano nchini.

Chama hicho kilikuwa kinaongea kufuatia kifo cha mwenzao Dkt Juma.

Katibu mkuu wa chama cha madaktari nchini Dkt Ouma Oluga, alishtumu serikali kwa kile alitaja kupuuzwa kwa madaktari wanaosomea Cuba.

Dkt Oluga alisema madaktari hao walioko ughaibuni wamekuwa wakilalamika kufuatia changamto wanazopitia nchini humo huku serikali ikifumbia macho.

Mazishi ya mwendazake inaendelea kupangwa huku familia, marafiki na wakazi wa Likoni wakiendelea kukutana nyumbani kwao kwa matayarisho hayo.

Dadake marehemu Bi Mishi Mboko alisema famlia inaendelea kutamaushwa na kifo hicho huku wakisubiri upasuaji au ripoti kutoka kwa serikali ambayo itabainisha kifo chake.