Manung’uniko tele Stars wakielekea Ghana AFCON

Na CHRIS ADUNGO

TIMU ya taifa ya Harambee Stars inatarajiwa kuondoka humu nchini hii leo kuelekea Ghana kwa marudiano ya mechi ya Kundi F ya kufuzu kwa fainali za Kombe la Afrika (AFCON) 2019.

Ingawa hivyo, kocha Sebastien Migne amedokeza kuhusu uwezekano wa kikosi hicho kufunga awamu mbili za safari baada ya suitafahamu ya fedha kutatiza juhudi za maandalizi.

Kufikia Jumatano, Shirikisho la Soka la Kenya (FKF) halikuwa limepokea fedha za kufadhili ziara ya Stars kutoka kwa Serikali.

“Timu ina kila sababu ya kuhofu serikali inapokuwa na mwendo wa kobe katika suala ya kuwadhamini Stars. Inakuwa vigumu kwa yeyote kutarajia matokeo bora kutoka kwa kikosi ambacho kwa hakika hakitendewi haki na washikadau muhimu,” akalalamika Migne akiwa mwingi wa fadhaa.

“Ilivyo, dalili zote zinaashiria kwamba itakuwa vigumu kuwakomoa Ghana ugenini,” akaongeza Migne kwa kuitaka Serikali kuchukulia kwa uzito maandalizi ya timu ya taifa kwa kutoa fedha kwa wakati ufaao.

Wakati huo huo, aliyekuwa kipa nambari moja wa Stars Arnold Origi amepata hifadhi mpya kambini mwa Helsingin HIFK kutoka Finland baada ya kuagana na Kongsvinger ya Norway.

Origi alijiunga na Sandnes Ulf ya Norway iliyomwajibisha mara 11 pekee mnamo Aprili 2018.

Kutua kwake HIFK kunamuunganisha na Wakenya Amos Ekhalie na Peter ‘Pinchez’ Opiyo ambao pia wanavalia jezi za kikosi hicho kitakachofungua kampeni za Ligi Kuu dhidi ya SJK mnamo Aprili 2019.

Kucheleweshwa kwa fedha ambazo zilikusudiwa kufanikisha maandalizi ya ziara ya Stars huenda kukayumbisha uthabiti wa Stars ambao kwa pamoja na wenyeji wao, wamefuzu kwa fainali za AFCON nchini Misri kati ya Juni 21 na Julai 19.

Stars wamepangiwa kuvaana na Ghana jijini Accra mnamo Machi 23 kabla ya kuelekea baadaye nchini Ufaransa kupiga kambi kwa kipindi cha majuma matatu ya kujifua.

Stars watakaokosa huduma za Olunga nchini Ghana, wameratibiwa kujinoa nchini Ufaransa kabla ya kutua Misri kwa fainali za AFCON.

Thomas Teye Partey wa Ghana audhibiti mpira usimponyoke kwa faida ya Mkenya Michael Olunga wakati timu hizo mbili zilimenyana Septemba 8, 2018, uwanjani Kasarani. Picha/ Kanyiri Wahito

Migne atalazimika kuzikosa huduma za mvamizi Michael Olunga atakapowaongoza vijana wake wa Stars kuchuana na Ghana.
Olunga alipata jeraha la paja alipokuwa akiwachezea waajiri wake Kashiwa Reysol dhidi ya Albirex Niigata katika Ligi Kuu ya Japan wiki mbili zilizopita.

Katika nafasi yake, Migne atamwajibisha fowadi matata wa Zesco United, Jesse Jackson Were aliyekosa kuunga orodha ya kikosi cha kwanza kilichoitwa kambini na Migne mwezi Februari 2019.

Sare au ushindi kwa Stars utawasaza kileleni mwa Kundi F.

Habari zinazohusiana na hii