Michezo

Huniambii chochote, Giggs amfokea Zlatan

March 21st, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MASHIRIKA

MANCHESTER, Uingereza

NYOTA mstaafu,Ryan Giggs amemfokea vikali Zlatan Ibrahimovic kwa madai kwamba winga huyo wa zamani alishirikiana na wenzake kuvuruga maisha ya kiungo Paul Pogba pale Old Trafford.

Ibrahimovic alikuwa amedai kupitia kwa gazeti moja la hapa nchini kwamba uhusiano mkubwa wa Giggs na wachambuzi wa soka Gary Neville na Paul Scholes ulimfanya kocha mkongwe, Sir Alex Ferguson kumchukia Pogba alipokuwa klabuni kwa mara ya kwanza.

Ibrahimovic alidai shutuma dhidi ya mwanasoka huyo mwenye umri wa miaka 26 zilianza mara tu alipoamua kuondoka Manchester United na kujiunga na Juventus mnamo 2012 wakati Ferguson akiwa usukani.

Alisema wachezaji hao wastaafu wametambuliwa kwa sababu waliichezea timu hiyo mechi nyingi, mbali na mataji mengi yaliyopatikana wakiwa kikosini.

Wachezaji hao wote ni miongoni mwa kikosi maarufu cha Class of 92, ambacho pia kilikuwa na Nicky Butt, David Beckham na Phil Neville ambacho kilicheza jumla ya mechi 3,450 wakati klabu hiyo ilijizolea sifa nyingi.

Ibrahimovic aliichezea Manchester mechi 53 baada ya kusajiliwa na Jose Mourinho mnamo 2016 kabla ya kuhamia LA Galaxy mnamo Machi 2018.

Mataji matatu

Giggs alisema ni jukumu la kila mchezaji wa zamani kuzungumzia hali ya klabu yake, huku akiwataka wachezaji walio klabuni humo leo wapigane vikali kufikia rekodi yao ya 1999, ambapo wakati huo Manchester ilitwaa mataji matatu ya Klabu Bingwa, Ligi Kuu ya Uingereza (EPL) na FA Cup.

Hakuna timu nyingine iliyoweza kusawazisha rekodi hiyo, lakini huenda Manchester City ikafaulu msimu baada ya kutwaa ubingwa wa Carabao Cup, wakati huu ikiendelea kufanya vizuri katika michuano ya Klabu Bingwa, EPL na FA Cup.

Katika shutuma zake, Ibrahimovic alishutumu kundi la baadhi ya wachezaji wa Class of ’92 kwa kujifanya wanaelewa Manchester United kuliko mtu mwingine.

Aliwataka nyota hao wastaafu waombe kazi klabuni badala ya kushutumu wachezaji mara kwa mara, lakini Giggs aliyeweza kuwa msaidizi wa David Moyes na pia Louis van Gaal klabuni hapo amemjibu.

“Unapoicheza Manchester United zaidi ya mechi 2000, unaweza kujilinganisha nasi na unakubaliwa kutoa maoni kuhusu klabu hiyo,” alimjibu kocha huyo wa timu ya taifa ya Wales kabla ya mechi ya kupimana nguvu dhidi ya Trinidad & Tobago.