Wanabodaboda wailetea Nairobi mapato ya Sh12 milioni
Na BERNARDINE MUTANU
Waendeshaji wa pikipiki wameendelea kuipa serikali ya Kaunti ya Nairobi fedha kwa kuvunja sheria.
Zaidi ya pikipiki 4,000 zimekamatwa na maafisa wa kaunti ya Nairobi tangu kupigwa marufuku katikati mwa Jiji mwaka jana.
Kutokana na hatua hiyo, Baraza la Jiji limepata Sh12.7 milioni kutokana na faini na ada za kuhifadhi zinazotozwa wamiliki wa pikipiki hizo kwa kukiuka marufuku.
Januari mwaka jana, Baraza la Jiji lilitoa agizo la kuruhusu pikipiki za uchukuzi wa kitaalam kufika katikati mwa Jiji. Wale wa kubeba abiria waliagizwa kuwa wakiwashukishia Ngara na City Stadium.
Marufuku hayo yalilenga kupunguza msongamano katikati mwa jiji na kudhibiti wahalifu.
Afisa wa usalama na utekelezaji Nairobi Tito Kilonzi alisema tangu marufuku hayo Mei 2018, jumla ya pikipiki 4,190 zilikamatwa kufikia Machi 4, 2019.
Alisema wamiliki wa pikipiki hizo walikamatwa kutokana na sababu tofauti ikiwemo ni pamoja na kufunga barabara, kuendesha pikipiki njia isiyofaa, kushusha wateja katika maeneo ambayo hayajakubaliwa na kuendesha pikipiki kwa njia za wapita njia.
“Faini za kortini zilikuwa jumla ya Sh2.68 milioni ilhali ada ya kuhifadhi pikipiki ilikuwa ni Sh9.8 milioni. Ada hiyo ni kati ya Sh1,000 hadi 80,000 kutegemea na kosa,” alisema.