Makala

FUNGUKA: 'Mume wa mtu raha sana…'

March 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na PAULINE ONGAJI

KATIKA uhusiano, sio wengi wanaopenda kulishwa sahani moja.

Hasa kwa mabinti wanaosaka waume, sio wengi wanaopenda kuwa nambari nyingine kama sio nambari wani.

Ndiposa wengi hung’atuka pindi wanapotambua kwamba kaka anayewavizia ana mke.

Lakini sio Ernesta, mrembo mwenye umri wa miaka 39, mkazi wa mojawapo ya mitaa ya kifahari jijini Nairobi.

Japo kapungukiwa kimasomo, kipusa huyu ana urembo wa hali ya juu, suala ambalo limemfanya kutamaniwa na madume wa haiba ya hali juu ambao mara kwa mara wametuma maombi ya kutaka kumposa.

Lakini Ernesta hana haja na madume vijana ambao yumkini hawajaonja utamu na uchungu wa ndoa.

Kipusa huyu amepiga nakshi ujuzi wake wa kuwavizia waume wa watu.

Na sio tu kuwavizia, mwanamama huyu anaponasa mume wa mtu anahakikisha kwamba ameshika mimba yake na kuzaa naye.

Ana watoto sita ambapo anakoishi inasemekana kwamba amezaa na zaidi ya wanaume sita wa watu.

Biashara

Anasema kwake tabia hii ni biashara kwani anatarajia pesa kila mwisho wa mwezi kutoka kwa madume hawa, huku akifyonza senti kutoka kwao.

Hiki ni kitega uchumi kwake ambapo kila mwanamume aliyemzalia humtumia Sh100,000 kila mwezi za matumizi.

Kama nilivyosema, mwanamama huyu ameumbwa akaumbika, suala ambalo asema limemchangia yeye kuzidi kupokea pesa kutoka kwa madume hawa.

“Jeni zangu ni za kipekee ndiposa madume wananifuata ili kuhakikisha kwamba pia wao wanapanda mbegu na kuvuna matunda yanayofanana nami.

Wanaume hawa wana pesa nyingi kwani kuna mfanyabiashara, mhasibu, daktari, meneja wa benki, mkaguzi mahesabu na mwanariadha.

Lakini hata wanaponisaidia hivi, nimeingia nao katika makubaliano kuwahakikishia usiri wao. Wote sita hawajuani na hakuna mtu mwingine anayejua kuhusu siri baina yangu na wao.

Kumbuka kuwa hawa ni wanaume ambao tayari wameoa na wana watoto lakini kutokana na sababu wanazofahamu, wanataka kupata mtoto nami.

Mmoja anasema kwamba mkewe ni kisura na amesoma lakini kamzalia madume tupu, na hivyo anataka kuzaa nami binti atakayefanana nami.

Mwingine naye asema mabinti ambao mkewe amezaa kidogo wamenyimwa umbo, na hivyo anataka nimzalie msichana mwenye umbo la chupa kama mimi.

Pia, kuna yule ambaye amevutiwa na ukarimu wangu kiasi cha kwamba anataka kuzaa nami binti mwenye moyo kama wangu.

La kushangaza ni kwamba Mungu amesikia maombi yao kiasi cha kuwa watoto wote niliozaa ni mabinti.

Kutokana na jinsi madume hawa wanavyonifaa, nimeamua kutoolewa kwani nikikubali kufanya hivyo, huenda nikawapoteza usaidizi ninaopokea, na  hivyo kupungukiwa na riziki.

Bado napanga kuzaa angaa watoto wanne zaidi nikitumia mbinu hii hii. Ujumbe wangu kwa wanawake walioolewa na hasa niliozaa na waume wao au wale ambao niko katika harakati za kushika mimba za waume wao, wasiogope kwani sina haja na uhusiano nao, ila tu nawasaidia kupata kipande cha uzuri wangu,” afunguka Ernesta.