Makala

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Nafasi ya sera katika upangaji lugha katika mataifa mbalimbali

March 23rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na MARY WANGARI

KWA mujibu wa Macdonald (1990) nchini Botswana walimu walikuwa na changamoto ya kimawasilino kwa kuwa na ujuzi mdogo wa kutumia lugha ya Kiingereza ambayo ndiyo lugha ya kufundishia elimu ya Sekondari.

Nchini Tanzania hali ni ngumu kwa walimu kama ilivyo kwa wanafunzi wa shule za upili. Kulingana na Rubagumya (2003), ni kwamba walimu wengi wa shule za sekondari nchini humo hawana uwezo wa kutumia lugha ya Kiiingereza kwa ufasaha, kufundishia badala yake huchanganya lugha ya Kiswahili na Kiingereza wakati wa kufundisha ili kurahishia ufundishaji.

Sera ya elimu inayohusu lugha ya kufundishia ndiyo mwongozo wa utayarishaji na utekelezaji wa mpango-lugha katika nchi husika. Massamba (2004) anahoji kwamba sera ya lugha ni maelezo rasmi au ya kisheria yanayohusu ukuaji na uendelezaji wa makusudi wa lugha katika jamii fulani ya watu.

 Kwa mujibu wa Massamba na wenzake (2011), Sera ni utaratibu wa kuendesha jambo kukidhi haja ya mamlaka na ndani ya sera,ndimo hutamkwa malengo,misingi na michakato ya uteuzi na utekelezaji wa jambo.

Kwa mantiki hiyo, sera ni mwongozo wa kufanya jambo kwa kadri ya mahitaji ya jamii ukibainisha malengo ya jambo linalotakiwa kufanywa, misingi yake na mchakato wa utekelekzaji.

Aidha, sera ya lugha ni jumla ya mawazo, matamko, sheria, kanuni na taratibu zenye kuelezea taratibu za utekelezaji wa mabadiliko ya nafasi na matumizi ya lugha katika jamii.

Vilevile, sera ya lugha ni matamko au maandishi kuhusu jinsi lugha zinavyopaswa kutumika katika jamii kwa kupeana nafasi ya majukumu katika jamii kama wanavyodai Massamba na wenzake

Uamuzi kuhusu lugha ya kutumia kufundishia ni wa muhimu kwa sababu lugha inaweza kuathiri mbinu na njia ya kufundishia kama wanavyosema Zhou na Sun (2004), kwamba katika mazingira ya Kiingereza kama vile Amerika, lugha ya kufundishia ni Kiingereza.

Kila anayehamia Amerika kutoka nchi nyingine anatakiwa kujifunza lugha ili aweze kuungana na wanafunzi wengine darasani. Aidha, Zhou na Sun wanafafanua  kwamba, lugha ya kufundishia katika shule zote za umma nchini Brazil ni Kireno cha Brazil.

 

Baruapepe ya mwandishi:[email protected]

Marejeo

Kothari, C. R. (2004). Research methodology Methods and Technique (Second Revised Edition). New Delhi: New Age International Publishers.

Koul L. (2009). Methodology of Educational Research (4th ed). New Delhi: Inda Vikas publishing House PVT Ltd.

Lambert, W. E. na wenzie (1960). “Evaluational Reactions to Spoken Languages”. Journal of Abnormal and Social Psychology. 20