Burundi yaingia AFCON 2019 kuongeza washiriki kutoka CECAFA kuwa timu tatu
Na GEOFFREY ANENE
BURUNDI imekuwa timu ya hivi punde kutoka eneo la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa) kutinga Kombe la Bara Afrika (AFCON) baada ya kupata alama moja iliyohitaji kufungia Gabon nje katika sare ya 1-1 Jumamosi mjini Bujumbura.
Timu ya Burundi inaungana na Kenya (Kundi F) na Uganda (Kundi L) katika AFCON itakayofanyika nchini Misri mwezi Juni/Julai mwaka 2019. Tanzania inaweza kuingia AFCON ikichapa viongozi wa Kundi F, Uganda.
Burundi na Gabon zilikamilisha dakika 45 za kwanza 0-0 kabla ya Burundi kutikisa nyavu za Gabon kupitia kwa mvamizi wa Al-Taawon, Cedric Amissi dakika ya 77.
Gabon, ambayo ilihitaji ushindi pekee kujikatia tiketi ya kuwa nchini Misri kwa AFCON mnamo Juni 21 hadi Julai 19 kutoka Kundi C, ilisawazisha kupitia kwa beki wa Burundi Omar Ngandu aliyejifunga dakika ya 82.
Baadhi ya majina makubwa yaliyokuwa katika kikosi cha Burundi ni Saido Berahino na Gael Bigirimana wanaosakata soka yao ya malipo katika klabu za Stoke City na Hibernian nchini Uingereza na Scotland, mtawalia.
Wawili hawa wote walikuwa na uwezo wa kuchezea Uingereza, lakini wakachagua Burundi, ambayo inashiriki AFCON kwa mara yake ya kwanza kabisa.
Burundi na viongozi wa kundi hili Mali walifuzu kushiriki AFCON, huku Gabon, ambayo ilikuwa inakaribisha mshambuliaji matata wa Arsenal, Pierre-Emerick Aubameyang, na Sudan Kusini zikiaga mashindano.
Sare kati ya Burundi na Gabon ilikuwa yao ya tatu mfululizo baada ya kutoka 0-0 mwaka 2014 na 1-1 mwaka 2018 katika mechi mbili zilizopita.
Burundi ni moja ya timu mpya kabisa katika AFCON 2019 zingine zikiwa ni Madagascar (Kundi A) na Mauritania (Kundi I). Kenya inarejea katika AFCON baada ya kukosa makala saba yaliyopita. Gabon iliandaa makala yaliyopita mwaka 2017.