Habari Mseto

Aliyebeba bangi apata ajali, anaswa na polisi

March 24th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

MACHARIA MWANGI na BENSON MATHEKA

Dereva aliyekuwa akisafirisha bangi alinusurika ajali ya barabarani lakiini akajipata katika mikono ya polisi gari lake lilipoanguka.

Dereva huyo alikuwa akiendesha gari kwa kasi kuepuka polisi gari lilipohusika kwenye ajali akapata majeraha na kuokolewa na maafisa hao.

Polisi walisema dereva huyo alipata majeraha mabaya baada ya gari alilokuwa akiendesha kugongana na gari lingine karibu na shamba la Delamare, kwenye barabara ya Naivasha kuelekea Nairobi.

Wakati wa kisa hicho cha saa kumi na moja na nusu alfajiri, watu wengine wawili walijeruhiwa na kukimbizwa katika Hospitali ya Naivasha Level Five ambako wanaendelea kutibiwa.

Kulingana na kamanda wa polisi wa Naivasha, Bw Samuel Waweru, dereva huyo alikuwa akisafirisha bangi na alikuwa akielekea upande wa Nairobi.

Alijaribu kupita gari nyingine kwa kasi ajali hiyo ilipotokea.

“Ilikuwa wazi kwamba dereva huyo alikuwa akiendesha gari kwa kasi kwa lengo la kuepuka polisi waliokuwa wakishika doria barabarani,” alisema mkuu huyo.

Hata hivyo, polisi waliofika eneo la ajali walikagua gari na kupata lilikuwa limebeba bangi

Bw Waweru alisema dereva huyo alikimbizwa katika hospitali ya Naivasha ambako anatibiwa chini ya ulinzi wa polisi.

Mwenzake alitoroka kwani hakujeruhiwa na polisi wanaendelea kumsaka.

Bw Waweru alisema bangi hiyo inakisiwa kuwa ya thamani ya Sh 1.5 milioni na ilikuwa ikisafirishwa hadi Mombasa kutoka eneo la Magharibi.

Mnamo Septemba mwaka jana, polisi walivamia boma la mlanguzi wa bangi na kupata magunia 11 na mawe 80 ya bangi iliyokadiriwa kuwa ya thamani ya Sh2 milioni.

Maafisa wa polisi walivamia boma hilo eneo la Kayole, nje ya mji wa Naivasha baada ya kudokezewa na wananchi.

Hata hivyo, mwenyewe alitoroka. Kisa hiki kinajiri siku moja baada ya polisi kumkamata mfanyabiashara wa Mombasa kwa tuhuma za kupatikana akisafirisha heroin kwenye gari lake.

Bw Abdulmajid Mselem Timami alikamatwa Ijumaa na polisi wakasema walipata akiwa ameficha kilo moja ya dawa hizo katika gari lake aina ya Honda.

Mfanyabiashara huyo anayemiliki malori kadhaa yanayobeba mizigo maeneo ya Afrika Mashariki anazuiliwa katika kituo cha polisi cha Central Mombasa akisubiri kufikishwa kortini.

Kulingana na polisi, thamani ya dawa alizodaiwa kupatikana nazo ni Sh1.5 milioni.