• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
Mvua sasa kuchelewa kufuatia kimbunga Idai

Mvua sasa kuchelewa kufuatia kimbunga Idai

 STEPHEN ODUOR Na BErNARDINE MUTANU

Idara ya Utabiri wa Hali ya Hewa imeonya kuwa mvua iliyotarajiwa kuanza mwezi huu itachelewa kutokana na kimbunga kilichokumba Msumbiji, Malawi na Zimbabwe.

Kulingana na utabiri wa hivi punde, idara hiyo inasema hali ya hewa imebadilika kutokana na kimbunga Idai kilichotokea wiki mbili zilizopita. Kulingana na idara hiyo, mvua ya masika imechelewa kwa sababu ya kimbunga ambacho kimeathiri msimu wa mvua hadi eneo la tropiki (ITCZ).

“Mvua ilitarajiwa kuanza katika baadhi ya maeneo nchini. Hata hivyo, kimbunga Idai kimeathiri msimu wa mvua nchini,” alisema Stella Aura, kaimu mkurugenzi mkuu wa huduma za utabiri katika Idara ya Utabiri wa Hewa.

Kulingana na taarifa hiyo, kimbunga hicho kilipunguza unyevu uliotarajiwa kufika nchini na kusababisha kuendelea kwa jua na hewa kavu katika maeneo mengi nchini.

Watu 1.1 milioni wanakabiliwa na tisho la kufa njaa kulingana na takwimu za Shirika la Msalaba Mwekundu nchini (KRC). Idara ya utabiri wa hali ya hewa nchini (KMD) inasema kwamba mvua ya masika inayotarajiwa kuanza baadaye mwezi huu haitakuwa ya kutosha maeneo mengi nchini.

Wakati huo huo waziri wa ugatuzi Eugene Wamalwa amesema serikali itaanza kugawa chakula cha misaada na kuzitaka serikali za kaunti kutenga pesa za kukabiliana na njaa katika bajeti ya ziada.

Bw Wamalwa alisema serikali kuu ilitarajia kuwa kaunti zilikuwa na mikakati ya kukabili njaa katika hatua za awali, lakini zikaishia kuikimbilia kama hatua ya kwanza.

“Kama serikali kuu tunafaa kuingilia kati wakati kaunti zimelemewa kwa kuwa zimetengewa pesa za kukabiliana na masuala spesheli,” alisema waziri huyo.

You can share this post!

Aliyebeba bangi apata ajali, anaswa na polisi

Shule za kibinafsi kimbilio licha ya gharama

adminleo