Habari Mseto

‘Nabii’ Owuor atabiri maafa zaidi Wakenya wasipotubu

March 25th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na BERNARDINE MUTANU

NABII David Owuor Jumapili alitabiri majanga zaidi ulimwenguni huku mataifa kadhaa ya eneo la kusini mwa Afrika yakiendelea kutatizika baada ya kukumbwa na Kimbunga kikali maarufu kama Idai.

Akihubiri wakati wa mkutano mkubwa uliofanyika katika bustani ya Central Park, Nairobi, Nabii Owuor alisema aliona katika ndoto dhoruba kali ulimwenguni kuliko kimbunga kinachoshuhudiwa nchini Msumbiji, Zimbabwe na Malawi.

Alisema kuwa alionyeshwa kimbunga kingine kitakachotokea Misri na kwingineko ulimwenguni na kuwataka watu kutubu.

“Tulipokuwa hapa mara ya mwisho, nilitabiri kuhusu mafuriko ulimwenguni. Kunayo dhoruba inayokuja duniani, dhoruba inakuja Misri na itakuwa kubwa zaidi,” alisema wakati wa mahubiri.

Kuhusu Kenya, mhubiri huyo alionya kuwa kuna adhabu inayokuja kwa Kenya kutokana na maovu yaliyokithiri.Alisema kuwa alizungumza na wakuu nchini na kuwaonya kuhusiana na umwangikaji wa damu Kenya ikiwa taifa halitatubu.

“Ninaona hukumu ya Bwana kwa Kenya; nilizungumza na viongozi wakuu kuhusiana na suala hilo ili kujitayarishia hili,” alisema.Dkt Owuor alisema kama alivyoonya kuhusiana na mapigano ya 2007, ndivyo anavyotabiri hali ya siku zijazo nchini.

“Kama nilivyoona 2005, 2006 na 2007, ilichapishwa na kusomwa na kila mmoja mpaka ikatendeka 2007. Nilionya kwamba niliona watu wakikimbilia maisha yao, niliona mapigano ya bunduki ila watu hawakunisikiliza mpaka ilipotendeka,” alisema na kuwataka wananchi kutubu.

“Mara hii tena, ikiwa shida yenu ni ukabila, lazima mtubu kuhusiana na hilo ili Mungu aiokoe nchi. Mara hii tena ninawaona mkikimbia tena huku risasi zikilia na hamna popote pa kutorokea,” alisema.

Kulingana na mwinjilisti huyo, ana ruhusa kutoka kwa serikali kupanga siku ya kitaifa ya toba itakayofanyika katika bustani ya Uhuru Park, Nairobi.

“Nilizungumza na wakuu zaidi kwamba tuandae siku ya kitaifa ya toba ili tuokoe taifa, la sivyo uovu mnaouona unaweza kupanuka na kuwa uovu wa kitaifa ambao unaweza kuharibu taifa hili zuri. Viongozi wakuu tayari wamekubali na kunipa ruhusa kujiandaa kuhusu siku hiyo,” alisema na kuwashauri viongozi wote kuhudhuria si tu kwa ajili ya kutubu lakini pia kupatana.

“Ikiwa hamtafanya hivyo, nimewaona mkikimbia kila mahali na damu nyingi ikimwagika. Ninaona kinachokuja na ni vyema nimeonyeshwa mapema kwa sababu kuna wakati mzuri wa kutubu,” alisema.

Alisema hayo wakati Kanisa analoongoza la Repentance and Holiness limekuwa likikosolewa sana kuhusiana na sakata kadhaa.