• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 6:50 PM
Asili ya majina ya ajabu ya mitaa mjini Nakuru

Asili ya majina ya ajabu ya mitaa mjini Nakuru

Na PHYLIS MUSASIA

NI kawaida kusikia miji yenye majina ya kushangaza. Kwa mfano mji wa Mombasa una mitaa kama Mwembe Tayari, Dongo Kundu, Uwanja wa Mbuzi, Kakuma, Dunga Unuse na kadhalika.

Mji wa Nakuru haujaachwa nyuma, ila majina yake yanashangaza.

Kusini mashariki mwa Ziwa la Nakuru, takribani kilomita tano kutoka katikati mwa jiji, upo mtaa kwa jina Shauriyako. Mtaa huu unamilikiwa na serikali ya Kaunti ya Nakuru ambako nyumba zilizojengwa huko ni za aina moja tu.

Wakazi wengi wa hapa ni waliokuwa wafanyikazi wa manispaa ya Nakuru kabla ya ujio wa serikali za kaunti nchini.

Shauriyako almaarufu Shauri, una nyumba za chumba kimoja kwa kila mkaazi au familia zinazoishi kule. Rosemary Kinyanjui; mama wa watoto wanne ambaye amekuwa mkazi wa hapa kwa zaidi ya miaka 25 anatueleza kuhusiana na jina la mtaa huu.

“Gharama ya maisha hapa si ghali, mtu yeyote wa kawaida anaweza kuishi huku na akae vyema bila kutatizika na majukumu ya hela. Nyumba ni za bei ya chini hata kwa Sh1,000 pekee utapata makazi,” akaeleza.

Anasema hapo nyuma ilikuwa kawaida ya watu wengi hasa waliokuwa wageni kutembelea mji wa Nakuru na kisha kuelekezwa kufika mtaa huo na kupata makazi ya kuishi. Kwa hivyo wamiliki wangesikika wakiwauliza kwamba “ni shauri ya hali yako wewe mwenyewe iliyokufanya uje huku kutafuta makazi?”

Baadaye kwa sababu ya mazoea hayo, mtaa huo ukapata jina hilo.

Kuna mtaa wa Ponda Mali ambao ni miongoni mwa mitaa duni. Pondaa kama vile wakazi wake wanavyouita, ni mtaa unaojishughulisha zaidi na mambo ya usafiri wa matatu kwani una steji ya magari mengi.

Kunalo pia soko kubwa ambako wakazi na hata watu wa nje wanaendeshea biasharara mbalimbali kama vile uuzaji wa nguo, mboga, kazi za juakali na uuzaji wa samaki na dagaa kwa bei nafuu.

Unapokaribia soko la Pondaa kilomita kama mbili hivi kutoka mtaa wa Kenlands, unakaribishwa na harufu nzuri ya samaki wanaochoma kwa mafuta. Ukiwa mwenyeji, utajua umefika nyumbani, na ukiwa mgeni, utafanya bidii kuifuata harufu hiyo ya samaki itakayokuelekeza hadi Ponda Mali.

Peter Nderegu Kariuki almaarufu Ponda Mali au Pondaa, 32, anaeleza kwa nini alipewa jina la mtaa huo.

“Nilipokuwa mdogo, kulikuwa na mzee fulani hapa ingawa alihamia mashinani. Alikuwa na duka la viatu lililokuwa limeandikwa Ponda Mali. Watu wote wa hapa wakawa wanamuita kwa jina hilo. Mzee huyo mara kwa mara angeniita na kunituma kwenye gala lake la viatu ili nimsaidie kazi ndogondogo,” akasema.

Baadaye alipohama kutoka mtaa huu, kijana huyu akarithi jina la mzee Ponda Mali na miaka 27 baadaye bado anafahamika kwa jina hilo.

Nilikutana pia na Titus Njuguna ambaye anajihusisha na biashara ya hoteli. Bw Njuguna anasema amekaa Pondaa kwa zaidi ya miaka 19 na kwamba jina hilo lilitokana na uzoefu wa watu wengi kwenda kwenye mtaa huo na kujivinjari kutokana na mali waliyokuwa nayo.

Kwenye eneobunge la Nakuru Mashariki, mabango yaliyo soko yanamkaribisha mgeni kwa maandishi ‘karibu soko mjinga’.

Nisijue pia wengi wa wafanyabiashara hao ni wakazi wa eneo hilo, Sharon Odhiambo mfanyabiashara wa dagaa.

“Wengi wetu tunaishi tu hapa nyuma. Kuna nyumba nyingi sana. Tunapofanya kazi mchana, jioni tunafunga na kuingia kwa nyumba zetu. Si mbali, unaweza kutembea hadi pale mwisho kisha uangalie upande wa kulia na kushoto utaona nyumba nyingi zikifuatana. Eneo hili lote ni makazi yetu,” akanieleza Bi Odhiambo huku akinyoosha mkono kwa ishara ya kunielekeza.

Mwendo mfupi kutoka Soko Mjinga nilifika Gikombaa. Hapa utapataa kila aina ya chochote unachohitaji.

Nilikutana na Terresia Warenga Kimani mfanyibiashara na pia mkazi wa Gikomba. Akanieleza kuwa, jinsi miji mingine kama vile Nairobi, Kisumu na Eldoret ilivyo na soko au sehemu fulani inayotambulika kwa jina la Gikombaa, pia Nakuru haijawachwa nyuma.

Nilimpata Bi Kimani akijishughulisha na biashara ya kuuza bidhaa za nyumbani kama vile sabuni ya mti na ile ya kupima ya unga, viberiti, dawa za meno miongoni mwa bidhaa nyingine kwenye kibanda chake kidogo.

Alisema hapo, ndipo. Na kwamba, ukifika Gikombaa umefika sehemu inayouza vitu vyote unavyokuwa ukihitaji. Kuna nguo za mitumba, maduka ya malimali, mboga za kienyeji, kuku, mayai na bidhaa nyingine kwa bei ya mtu wa kawaida. Wakati mwingi utawasikia wakazi wa hapa wakiuita mtaa wao “okoa jahazi” kutokana na aina ya bidhaa zinazouzwa na pia bei yazo nafuu.

Mtaa mwingine ni London. Tofauti sana na mji wa London kule Uingereza, London ya Nakuru ndio mtaa unaokaribisha aina zote za taka zinazosafirishwa na malori ya kaunti hadi jaa kuu la Gioto.

Huku, nikiwa na mwanahabari mwenza Bw Richard Maosi, tulikutana na mlima mkubwa wa taka zilizomwagwa sehemu hii. Inasemekana kuwa eneo kuu la taka inayokusanywa kutoka mji wote wa Nakuru.

Harufu mbaya huku, kwa wakaazi wa London na Hilton ni jambo la kawaida. Bi Keith Mboko mkaazi wa mtaa huu ambaye amekuwa hapa kwa takribani miaka 13 alitueleza kuwa ukiwa mgeni katika mji wa Nakuru, na usikie kuhusu mtaa wa London, utadhai ni eneo la matajiri wote na wenye vyeo kubwa kubwa kwenye kaunti hiyo. Lakini la, unapofika London habari ni tofauti sana.

Usalama katika mtaa huu unazua wasiwasi si haba. Vijana ambao wameteka nyara eneo lote la taka la Gioto wanawaangaisha sana wakazi wa London na Hilton. Usiku na mchana wakazi wanalalamika kupoteza mali yao kwa kupigwa ngeta hadharani. Na wakati wa usiku pia wanatumia nguvu kuvunja milango za wakazi kabla ya kuingia ndani na kuwapora.

Bw Festus Langat aliyekuwa mkuu wa maswala ya posta kabla ya kustaafu, alitueza amekaa London kwa zaidi ya miaka kumi na kulingana naye, hali ya usalama katika sehemu anayoishi imeimarika ikilinganisha na miaka ya hapo hawali.

Hata ingawa tulikutana naye nyumbani kwake akiwa anaangaia jinsi sehemu moja ya ua linalozunguka nyumba yake lilivyobomolewa usiku wa kuamki siku hiyo, bado anashikilia kauli kwamba usalama huko umekuwa afadhali.

“Yale madhara waliokuwa wakitufanyia vijana wa kutoka Gioto pale juu, siwezi kulinganisha na uharibifu huu ninaouona hapa. Mambo yalikuwa mabaya sana,” akasema.

Alisema taa zote zilizokuwa zikiwekwa juu ya milingoti za stima zilikuwa zikivunjwa ili kuwapa muda mwafaka wa kufanya maovu wao.

London ni sehemu pia inayopendwa na wanafunzi wengi kwa sababu bei ya nyumba kule ni nafuu.

Lakini Bw Langat anasema, tayari kuna kesi kortini iliyowasilishwa na wakazi wa Londoni kupinga ujenzi Zaidi wa vyumba vya kulala kwa wanafunzi kwa sababu vinakaribisha majambazi wengi wanaoendelea kuwaangaisha kwani wengi wao wanajifanya wanafunzi na kukodisha vyumba hivyo.

Alisema jina la London lilianzishwa kutokana na mtu mmoja mwenye asili ya kiingereza aliyekuwa amejenga nyumba yake kwenye sehemu moja ya mtaa huo na kuibandika jina la White House London.

Kwa sababu ya hiyo, kukaibuka mitaa miwili tofauti inayopakana sehemu hiyo na kujipatia majina ya London na White House mtawalia.

Unapo ondoka mji wa Nakuru ukitumia barabara inayokuelekeza katika eneo la jumba la biashara la West Mall Nakuru magharibi, kilomita mbili hivi kutoka eneo hilo unafika katika mtaa mwingine kwa jina Shabab. Wengi ambao ni wageni Nakuru hubaki kujiuliza mbona Shabab kutokana na umaarufu wa kundi la kigaidi nchini Somalia kwa jina Al Shabaab.

Shabab ya Nakuru haihusiki kwa vyovyote vile na kundi ya kigaidi la Al Shabaab. Na huku unakaribishwa na idadi kubwa ya gereji zinazofanya kazi yake kando kando ya barabara kuu ya mtaa mzima.

Bw Paul Waweru ambaye ni mkazi wa Shabab tangu utotoni hadi sasa amekuwa mzee mzima, alinieleza kuwa wingi wa gareji Shabab unatokana na idadi kubwa ya dungu wengi wa kutoka eneo la Nyanza.

Kelele za mashine ya kuchomelea vyuma pamoja na kugonga mabati kwa marekebisho ya magari, tinga na pikipiki ni jambo la kawaida mtaani Shabab.

Waweru aidha alinieleza kuwa hapo zamani za kale kuliishi jamii kubwa ya watu wa asili ya kiindi katika mtaa huo. Kukatokea kwamba kulikuwa na jamii moja katika yao iliofahamika kama shabab. Hata walipokuwa wakitembea ungewasikia wakitambuana kwa jina hilo na ndipo wakazi wakaanza kuwa na uzoefu walo jambo lililopelekea mtaa mzima kupata jina la kipekee. Wakaziwa hapa utawasikia wakiita Shabee badala ya Shabab.

Mitaa nyingine Nakuru ni kama vile Bahati, Langalanga, Bondeni, Lanet, Kanu Street, Eveready, Kaptembwa miongoni mwa mitaa nyingine.

You can share this post!

Mbunge ataka Matiang’i ajiuzulu, asema hawezi kazi

Wakenya hawataki mzigo zaidi – Utafiti

adminleo