Habari

Wasamaria kutoka kuzimu

March 26th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na VALENTINE OBARA

TABIA ya wahisani kutoka ng’ambo kuwadhulumu watoto mayatima na wanaotoka familia maskini, imefikia upeo mpya baada ya Idara ya Upelelezi ya Amerika (FBI) kuanza kuchunguza mume na mkewe kwa madai ya unajisi katika makao ya watoto Bomet.

FBI inachunguza raia wake wawili, Gregory Dow na mkewe Mary Rose, kwa madai ya kudhulumu watoto kimapenzi katika makao ya watoto waliyosimamia katika eneo la Boito.

Ufichuzi huu umetokea siku chache baada ya mahakama kuagiza makao ya watoto ya Martyrs of Uganda katika Kaunti ya Machakos

ifungwe, baada ya kufichuliwa wavulana katika makao hayo wamekuwa wakilawitiwa.

Ingawa wavulana karibu tisa walilalamika kuhusu ulawiti waliotendewa na mpishi wa kiume, hakuna hatua zilichukuliwa hadi watetezi wa haki za binadamu walipoingilia kati.

Ongezeko la visa hivi limefanya Idara ya Kuchunguza Uhalifu (DCI) kuanzisha kitengo kipya cha kupambana na dhuluma dhidi ya watoto.

Mkurugenzi Mkuu wa shirika lisilo la kiserikali la Kenya Alliance for Advancement of Children, Bw Timothy Ekesa alisema hatua za dharura zinahitaji kuchukuliwa.

“Ukichunguza vyema utakuta visa vingi huwa haviripotiwi kwa sababu wahusika hutoa vitisho,” akasema mwanasaikolojia wa watoto, Bi Loice Okello.

Kwa miaka kadhaa sasa, kumekuwa na visa zaidi ya saba ambapo raia wa kigeni wamechunguzwa na baadhi kupatikana na makosa ya kudhulumu watoto katika makao ya mayatima.

Mwaka jana, Hans Egon Dieter Vriens, ambaye ni raia wa Uholanzi alikamatwa na maafisa wa Idara ya Upelelezi wa Jinai (DCI) kwa kubaka wasichana wa umri wa kati ya miaka minane na kumi.

Ilisemekana kulikuwa na wasichana wanane waliokuwa wakiishi nyumbani kwake wakipokea misaada kama vile elimu.

Mwaka huo huo, Keith Morris, 72, ambaye ni raia wa Uingereza, alipatikana na hatia ya kudhulumu wasichana kimapenzi na akahukumiwa miaka 18 na miezi sita gerezani Uingereza.

Mapema 2011, Kasisi Kizito wa Kanisa Katoliki aligonga vichwa vya habari kwa madai ya kudhulumu watoto kimapenzi katika makao ya watoto aliyosimamia mtaani Dagoretti. Hata hivyo, wavulana waliohusika baadaye walidai walilazimishwa kumharibia sifa kasisi huyo.

Mnamo 2015, Mwingereza Simon Harris alihukumiwa miaka 17 na miezi minne gerezani na mahakama ya Uingereza iliyompata na hatia ya kulawiti wavulana wa kurandaranda mitaani katika eneo la Gilgil.

Mwingereza mwingine, Simon Wood, alijitoa uhai 2014 alipokumbwa na mashtaka ya ubakaji wa wasichana wenye umri wa kati ya miaka mitano na 13, alipokuwa akitoa misaada katika shule na makao mbalimbali ya watoto Kenya, Uganda na Tanzania.

Nchini Amerika, Matthew Lane Durham, aliyekuwa na umri wa miaka 21 alihukumiwa miaka 40 gerezani kwa kudhulumu watoto kimapenzi katika makao ya mayatima ya Upendo jijini Nairobi, kati ya Aprili na Juni 2014.