Wakenya hawataki mzigo zaidi – Utafiti
Na PETER MBURU
WAKENYA wengi hawataki kuongezewa mzigo wa uongozi kwenye kura ya maamuzi, asilimia kubwa wakipendekeza baadhi ya viti vya uwakilishi vilivyopo sasa, aidha viondolewe ama vipunguzwe.
Hii ni kulingana na utafiti uliofanywa na mashirika ya Infotrak na Integrated Development Network (IDN).
Utafiti huo umeonyesha kuwa japo wengi wa Wakenya wanataka katiba ifanyiwe marekebisho, lengo lao ni viti vya uwakilishi kupunguzwa ili mzigo wa mishahara ndani ya serikali uthibitiwe.
Utafiti huo ambao ulichapishwa jana, ulisema kuwa asilimia 65 ya Wakenya wangetaka katiba ifanyiwe marekebisho huku asilimia 52 kati yao wakisema hilo litasaidia kurekebisha mapengo kwenye katiba na asilimia 38 wakitaka irekebishwe ili kupunguza wajumbe wanaowakilisha wananchi.
Vilevile, utafiti huo ulisema kuwa asilimia 56 ya Wakenya wanapinga kuundwa kwa viti vya Waziri Mkuu pamoja na manaibu wake wawili, ama mfumo wa serikali ambapo wabunge watamchagua kiongozi wa serikali.
“Wakenya wengi (asilimia 72) kutoka maeneo manane wanapendelea uongozi wa Urais na wangependa kujichagulia Rais wanayemtaka moja kwa moja,” utafiti huo ukasema.
“Wanaounga mkono serikali ambapo wabunge watamchagua kiongozi wa serikali ni asilimia 18 ya Wakenya, uungwaji mkono zaidi ukiwa maeneo ya Nyanza na Pwani kwa asilimia 28 na 22 mtawalia,” Mtafiti Mkuu wa Infotrak Walter Nyabundi akasema.
Wakenya wengi pia walipendekeza viti vya uwakilishi wa wanawake na maseneta kuondolewa, na idadi ya kaunti na maeneo bunge kupunguzwa kama mbinu ya kuthibiti mzigo wa mishahara ya umma ambao unazidi kuilemea serikali.
Hata hivyo, Wakenya walionekana kutetea viti vya wawakilishi na maafisa wa serikali wa ngazi za chini, wakipinga kuondolewa kwa viti vya madiwani ama kuvunjwa kwa serikali za utawala.
“Wakenya bado wanafurahia umuhimu wa usimamizi wa utawala na hivyo wengi wao wanapinga kuvunjwa kwa afisi za chifu na Makamishna wa Kaunti,” akasema Bw Nyabundi.
“Asilimia 67 ya Wakenya wangependa ugatuzi kuimarishwa kwa serikali za kaunti kupewa rasilimali zaidi. Vilevile, Wakenya wengi (asilimia 59) wanapinga mapendekezo ya katiba kuondoa kiti cha udiwani.”
Hata hivyo, asilimia 38 ya Wakenya waliunga mkono kiti hicho kuondolewa kwenye katiba.
Wakenya aidha walieleza pingamizi zao kuhusu pendekezo la aidha kubadili uongozi wa Urais kutoka mihula miwili ya miaka mitano kila mmoja, ama kuondoa vidhibiti vya muda wa uongozi wa Urais.
Asilimia 57 walipinga mfumo wa uongozi ambao Rais ataongoza kwa muhula wa miaka saba, nao asilimia 65 wakapinga kuondolewa kwa vidhibiti kuwa Rais aongoze kwa mihula miwili pekee.
Zaidi ya thuluthi mbili ya Wakenya waliunga mkono kuundwa kwa afisi ya kiongozi wa upinzani bungeni na katika seneti, nao asilimia 58 wakapendekeza uchaguzi mkuu kuwa ukiandaliwa Desemba, badala ya Agosti.
Utafiti huo ulifanywa kati ya Februari 9 na 11, ukihusisha kaunti 15, ambapo watu 800 walihojiwa. Kati ya Wakenya waliopinga wito wa kura hiyo ya maamuzi, asilimia 33 walisema hakuna haja ya kuiandaa, nao asilimia 32 wakasema shughuli hiyo itakuwa ghali.
“Asilimia 27 kati yao walihisi kuwa zoezi hilo linalenga kunufaisha wanasiasa tu,” ripoti hiyo ikaongeza. Asilimia 32 walisema haina maana, nao asilimia 30 wakasema ni ghali.