Hoja ya kumtimua Ruto ni njama ya Raila kuwa Naibu Rais – Jubilee
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE 15 wa Jubilee wameshutumu kiongozi wa ODM Raila Odinga wakidai ndiye anamchochea Seneta wa Siaya James Orengo kuwasilisha hoja bungeni ya kumtimua afisini Naibu Rais William Ruto.
Wakiongozwa na Mbunge wa Kiharu Ndindi Nyoro, wabunge hao ambao ni wandani wa Naibu Rais walidai kuwa nia ya Bw Odinga ni kutwaa wadhifa huo wa Dkt Ruto, ambayo walisema haitafaulu.
“Tunajua Orengo ni mtu wa mkono wa Odinga. Raila ndiye anataka kumtumia kumng’oa Naibu Rais William Ruto ili achukue kiti hicho kwa njia ya mkato. Lakini tunataka kumwambia kwamba Jubilee iko imara na mipango hiyo kamwe haitafaulu,” akasema Jumanne kwenye kikao na wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.
“Tunataka kumwambia Raila kwamba njia ya kipekee ya kupata mamlaka ni kupitia kujiwasilisha kwa wananchini ili apigiwe kura. Sio kutumia Orengo kuwasilisha hoja isiyo na mihilimi kikatiba,” akaongeza Bw Nyoro ambaye anahudumu bungeni kwa muhula wa kwanza.
Naye Mbunge wa Kimilili Didmus Barasa alidai kuwa lengo kuu la Bw Orengo ni kuing’oa mamlakani serikali ya Jubilee inayoongozwa na Rais Uhuru Kenyatta.
“Hii hoja hailengi Ruto pekee bali lengo Rais Kenyatta kwa sababu wawili hao walichaguliwa kwa tiketi moja katika chaguzi kuu zilizopita. Na hivi vita vya ufisadi vinalenga kusambaratisha serikali ya Jubilee, ” akasema Bw Barasa.
Wabunge hao walidai kuwa Dkt Ruto anaungwa mkono na asilimia 90 ya wabunge katika Bunge la Kitaifa na Seneti wakisema hiyo ni ishara tosha kwamba hoja ya Bw Orengo itafeli.
“Tunataka kumwambia Orengo kwamba Ruto anashabikiwa na zaidi ya asilimia 90 ya wabunge katika mabunge yote mawili. Kwa hivyo akome kumhadaa Raila kwamba hoja yake itapita,” akasema Mbunge Mwakilishi wa Laikipia Bi Catherine Waruguru.
Wengine waliohudhuria kikao hicho cha wanahabari ni; Nixon Korir (Langat), Joyce Korir (Mbunge Mwakilishi wa Bomet), Tecla Tum (Mbunge Mwakilishi wa Nandi), Caleb Kositany (Soy), Silvanus Osoro (Mugirango Kusini) na John Waluke wa Sirisia.
Wangine walikuwa; Kipsengeret Koros (Sigowet/ Soin), Mathias Robi (Kuria Magharibi), Benjamin Gathiru (Embakasi ya Kati) na Gideon Keter (Mbunge Maalu).
Wabunge hao walimrushia Bw Odinga matusi machafu, wakiapa kuwa kamwe hatafanikisha ndoto yake ya kuwa Rais wa tano.
“Tunahakika kwamba Dkt Ruto atamshinda tena mnamo 2022. Hii ndio maana anapanga njama chafu ya kumng’oa mamlakani,” akasema Bw Osoro ambaye alichaguliwa bungeni kwa tiketi ya chama cha KNC.
Mwishoni kwa wiki Bw Orengo alisema anasaka uungwaji mkono kutoka kwa wabunge wa NASA na wale wa Jubilee pindi atakapowasilisha hoja hiyo.
“Ikiwa Ruto amekataa kujiuzulu nitamwondoa kupitia kura ya hoja bungeni kuwa kuzingatia kipengee cha 150 (1) (b) linachotoa mwanya kwa Naibu Rais kuondolewa mamlakani kutumia mchakato wa kisiasa,” akasema Bw Orengo alipohutubia mkutano wa kampeni katika eneo bunge la Ugenya.
Lakini Bw Orengo atakuwa na kibarua kikubwa endapo ataandaa hoja hiyo. Ni sharti apate uungwaji mkono wa angalau thuluthi moja ya wabunge katika bunge la kitaifa (yaani wabunge 177).
Sababu za kuondolewa kwa Naibu Rais sharti ziwe ni ukiukaji wa Katiba au sheria yoyote ile au mienendo mibaya.
Hoja hiyo ikiidhinishwa na Spika, sharti bunge liitishe mkutano wa maseneta wa kusikiza madai dhidi ya Ruto. Baadaye kamati ya maseneta 11 itaundwa kuchunguza madai ya Orengo dhidi ya Naibu Rais.
Kamati hiyo pia itamwita Ruto kujitetea mbele yake na endapo itabaini kuwa madai ya Orengo yana mashiko, Seneta huyo atahitaji uungwaji mkono wa angalau thuluthi mbili ya wabunge na maseneta ili kufaulu kumwondoa Ruto mamlakani.
Hiki ni kibarua kigumu ikizingatiwa kuwa Dkt Ruto ana ufuasi mkubwa ndani na nje ya bunge kando na uwezo wake mkubwa kifedha.