• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
GWIJI WA WIKI: Amidah Khalekha

GWIJI WA WIKI: Amidah Khalekha

Na CHRIS ADUNGO

MUNGU alipokuumba, alikupa kipaji ambacho aliwanyima wengine.

Kuanzia leo jipende, jikubali, jizungumzie, jisake upya na jitabirie mambo mazuri.

Jihisi kuwa mwenye thamani na kataa kujilinganisha na mtu mwingine.

Usikubali kushindwa na jambo lolote maishani. Katika kila ufanyacho au unachotarajia kufanya, ukitanguliza mawazo ya kushindwa, haitakuwa rahisi kufaulu.

Fikra anazokuwa nazo mtu kuhusiana na jambo fulani ndizo humpa msimamo na mtazamo maishani.

Mawazo anayokuwa nayo mtu kwa muda mrefu huwa yanajitokeza katika maneno na hatimaye matendo yake.

Kwa hiyo, badilisha jinsi unavyowaza kuhusu hali yako.

Tupo kama tulivyoamini kwamba tupo. Ukiamini wewe ni tajiri, basi wewe ni tajiri! Ukiamini huwezi kufanya jambo ni kweli hutaweza! Ipo nguvu kubwa ajabu katika kuamini!

Huu ndio ushauri wa Bi Amidah Khalekha – mshairi shupavu na mwandishi chipukizi wa Kiswahili ambaye kwa sasa ni Mkuu wa Idara ya Lugha katika Shule ya Upili ya Khwisero Girls, Kakamega.

Maisha ya awali

Amidah alizaliwa mnamo Machi 1986 katika kijiji cha Lumakanda, eneo la Lugari, Kaunti ya Kakamega akiwa mtoto wa sita kati ya saba katika familia ya Bw Issah Wekhui Mchelule na Bi Mwanahawa Agnetta Wekhui.

Alianza safari yake ya elimu katika Shule Msingi ya Lumakanda Township, Lugari alikosomea kati ya 1993 na 2000.

Alama nzuri alizozipata katika mtihani wa KCPE zilimpa nafasi ya kujiunga na Shule ya Upili ya Archbishop Njenga Girls High, Kakamega mnamo 2001.

Alihitimu Hati ya Masomo ya Sekondari (KCSE) mwishoni mwa mwaka 2004.

Miaka miwili baadaye, alijiunga na Chuo Kikuu cha Moi, Eldoret kusomea Shahada ya Elimu (B.Ed Arts).

Akiwa huko, aliwahi kuwa kinara wa Chama cha Kiswahili katika Chuo Kikuu cha Moi (CHAKIMO) na Chama cha Wanafunzi wa Kiswahili katika Vyuo Vikuu vya Afrika Mashariki (CHAWAKAMA).

Haya ni majukwaa yaliyompa fursa ya kuwasilisha makala ya kitaaluma katika makongamano mengi ya kitaifa na kimataifa.

Alihitimu na kufuzu kuwa mwalimu wa Kiswahili na somo la Jiografia mnamo 2010.

Anatazamia sasa kurejea chuoni mwishoni mwa mwaka huu na kukizamia Kiswahili katika kiwango cha shahada za Umahiri na Uzamifu.

Amidah anatambua ukubwa wa mchango wa wazazi wake katika kumwelekeza vilivyo, kumshauri ipasavyo na kumtia katika mkondo wa nidhamu kali.

Aliyemshajiisha zaidi kujitahidi masomoni akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi ni Mwalimu Joash Sirengo ambaye kwa sasa ni mstaafu.

Anakiri kuwa ukubwa wa mapenzi yake ya dhati kwa taaluma ya ualimu ni zao la kuhimizwa na kuhamasishwa pakubwa na Bw Bramwel Fula Kamwani aliyekuwa mwalimu wake katika shule ya upili.

Kariha na ilhamu zaidi ilichangiwa na wahadhiri waliotangamana naye kwa karibu sana, kumpokeza malezi bora ya kiakademia na kupanda ndani yake mbegu zilizootesha utashi wa kukichangamkia Kiswahili alaa kulihali akiwa mwanafunzi wa Shahada ya Kwanza katika Chuo Kikuu cha Moi (Bewa Kuu), Eldoret.

Mbali na Dkt Collins Kenga Mumbo, Dkt Saidi Vifu Makoti na Profesa Nathan Oyori Ogechi, mwingine aliyemchochea pakubwa kwa imani kuwa Kiswahili kina upekee wa kumwandaa mtu katika taaluma yoyote na kwamba lugha hiyo ni kiwanda kikuu cha maarifa, ajira na uvumbuzi ni marehemu Profesa Naomi Luchera Shitemi ambaye hadi kufariki kwake, alikuwa msomi mtajika wa taaluma ya Tafsiri.

Mtihani mgumu zaidi ambao Amidah alikabiliana nao baada ya kukamilisha mtihani wake wa KCSE ni vita vya ndani ya nafsi vilivyompa msukumo wa kutaka kujitosa kikamilifu katika ulingo wa Kiswahili na kuwa ama mwanahabari stadi, mwalimu mashuhuri, mwandishi maarufu au mtunzi shupavu wa mashairi.

Ualimu na uanahabari ni taaluma ambazo Amidah alivutiwa kwazo tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi, japo watoto wengi wa hirimu yake walikosa kabisa kuona thamani ya ndoto hizo za mwenzao kwa wakati huo.

Kwa hakika, ufanisi unaojivuniwa na Amidah kwa sasa katika ulingo wa Kiswahili unatokana na tukio la yeye kufundishwa na wasomi ambao mbali na kubobea ajabu kitaaluma, pia waliipenda na kutawaliwa na ghera ya kuipigia chapuo lugha hiyo.

Ualimu

Amidah alianza kufundisha Kiswahili na Jiografia katika Shule ya Upili ya Bunyore Girls, Vihiga mnamo 2009. Alihudumu huko kwa kipindi kifupi kabla ya kuhamia Delamere Girls, Nakuru mwanzoni mwa 2010.

Akiwa huko, aliamsha ari ya kuthaminiwa kwa Kiswahili miongoni mwa wanafunzi na walimu wenzake shuleni humo.

“Wanafunzi walianza kushiriki mashindano ya uigizaji na kughani mashairi katika tamasha za kitaifa za muziki na drama. Jambo hili lilibadilisha pakubwa sura ya kusomwa na kufundishwa kwa Kiswahili, nao walimu wakapata hamasa zaidi.”

Mnamo 2012, alirejea Archbishop Njenga Girls, mara hii kwa lengo la kuwapiga msasa wanafunzi wa shule hiyo na kuwatandikia zulia zuri la Kiswahili.

Baada ya kipindi kifupi, aliajiriwa na Tume ya Huduma kwa Walimu (TSC) iliyomtuma katika Shule ya Khwisero Girls, Kakamega.

Kwa sasa, yeye ni Mlezi wa Chama cha Kiswahili, Mkuu wa Idara ya Lugha shuleni humo na mwamuzi wa kiwango cha kaunti kwenye tamasha za kitaifa za muziki na drama.

Anaungama kwamba kufaulu kwa mwanafunzi yeyote hutegemea pakubwa mtazamo wake kwa masomo anayofundishwa na kwa mwalimu anayempokeza elimu na maarifa darasani.

Amidah anajivunia tajriba pevu katika utahini wa Insha ambayo ni Karatasi ya Kwanza ya KCSE Kiswahili (KAR 102/1).

Anasisitiza kuwa jitihada zisizokadirika pamoja na ushirikiano mkubwa kati yake na walimu wenzake katika Idara ya Lugha shuleni Khwisero Girls ni nguzo kubwa katika ufanisi wanaojivunia kila mara matokeo ya mitihani ya kitaifa ya KCSE yanapotangazwa.

Uzoefu katika utahini umwezesha kuzuru shule mbalimbali za humu nchini kwa nia ya kukipigia chapuo Kiswahili na kuwahamasisha walimu na wanafunzi kuhusu mbinu mwafaka zaidi za kujiandaa kwa mitihani ya KCSE.

Zaidi ya kuhudhuria makongamano mbalimbali katika jitihada za kuchangia makuzi ya Kiswahili, Amidah amewahi pia kualikwa kufundisha, kuwashauri na kuwaelekeza walimu na wanafunzi katika shule mbalimbali za msingi na za upili ndani na nje ya Kaunti ya Kakamega.

Aidha, anajivunia kuchangia kishujaa uendeshaji wa kipindi ‘Mawanda ya Lugha’ katika Idhaa ya Radio Kisima. Anakiri kuwa umilisi alionao na upekee wake wa lugha ni zao la kushiriki kipindi hiki ambacho huangazia vipengele anuwai vya Fasihi ya Kiswahili.

Uandishi

Amidah anaamini kwamba safari yake katika uandishi ilianza tangu akiwa mwanafunzi wa shule ya msingi.

Nyingi za insha na mashairi aliyoyatunga yalimzolea sifa na kumvunia umaarufu miongoni mwa mwenzake.

Isitoshe, ufundi mkubwa katika tungo alilzozisuka ni upekee uliompandisha kwenye majukwaa ya kila sampuli ya kutolewa kwa tuzo za haiba kubwa na za kutamanika mno katika ulingo wa Kiswahili.

Mnamo 2019, alichapishiwa Mwongozo wa ‘Chozi la Heri’. Hiki ni kitabu alichokiandika kwa ushirikiano na mwalimu Henry Mokua wa Shule ya Upili ya Nyamira Boys na mwalimu John Nyandwarwo ambaye kwa sasa anafundisha katika Shule ya Upili Nyorangi Mixed, Kaunti ya Migori.

Jivunio

Anapojitahidi kufikia upeo wa taaluma yake na kuweka hai azimio la kuwa Profesa, Amidah anajivunia kufundisha idadi kubwa ya wataalamu ambao kwa sasa wanashikilia nyadhifa za hadhi katika sekta mbalimbali ndani na nje ya ulingo wa Kiswahili.

Baadhi yao ni Halima Shoba na Hellen Asiko ambao wamepania kuzifuata nyayo za mwalimu wao.

Kwa imani kwamba mfuko mmoja haujazi meza, Amidah pia ni mfanyabiashara mjini Kakamega.

Kwa pamoja na mumewe Al-Imran Dianga, wamejaliwa watoto wawili: Faleysah Kenda na Noor Andama.

You can share this post!

Yafichuka raia wa kigeni 35,000 wamepata kazi Wakenya...

KAULI YA WALIBORA: Kongamano kuhusu ugaidi Iraki...

adminleo