• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 9:15 PM
NDIVYO SIVYO: Neno ‘kaa’ halipaswi kamwe kutumiwa katika ulinganishi

NDIVYO SIVYO: Neno ‘kaa’ halipaswi kamwe kutumiwa katika ulinganishi

Na ENOCK NYARIKI

BAADHI ya watu hukitumia kitenzi kaa wakati wa kulinganisha watu wawili au vitu viwili vyenye sura, maumbo au tabia zinazokaribiana.

Wengine hulitumia badala ya ‘kama’ ambalo linapotumiwa katika usemi huibua dhana ya shaka.

Unakaa ‘krimino’

Neno hili aghalabu hutumiwa hivyo na watu wa jinsia ya kike. Ni vigumu hata hivyo kutoa sababu zinazolifanya neno hilo kuzunguka mazungumzo ya jinsia tuliyoitaja. Zifuatazo ni kauli zinazotokana na matumizi hayo:

Mwanamasumbwi huyu anakaa mwanamume.
Mtu huyu anakaa mwizi.
Juma anakaa dada yake.

Sentensi ya kwanza inaibua dhana ya mshabaha au mfanano.

Kwamba sura au umbo la mwanamasumbwi anayezungumziwa linamdhihirisha kuwa mwanamume ijapokuwa yeye ni mwanamke.

Sentensi ya pili inazua dhana ya shaka. Mzungumzaji anamshuku mtu mwenyewe kuwa mwizi.

Sentensi ya tatu nayo inaibua dhana ile ile inayojitokeza katika sentensi ya kwanza.

Katika sentensi zote tatu, neno kaa limetumiwa visivyo. Waama, halipaswi kutumiwa katika ulinganishaji wa watu au vitu.

Linapotumiwa kama nomino huzua fasili tatu muhimu.

Kwanza, ni kipande cheusi cha ukuni kinachochomwa na kuzimwa kabla ya kuwa majivu. Pili, ni kipande chekundu cha ukuni kinachotoa moto.

Tatu, ni mnyama mdogo wa majini mwenye miguu zaidi ya sita na gamba mwilini. Mnyama huyu hujitokeza katika methali: Kaa akiinua gando, mambo yamekatika.

Katika methali hii, mtu mwenye tajriba au uzoefu wa kazi fulani na ambaye huitenda kwa wepesi amelinganishwa na kaa ambaye ni mwepesi wa kushika windo lake kwa kutumia gando lake.

Mojawapo ya fasili tano za kitenzi kaa ni ile ya kitu kuwa na mwonekano wa nje wa kupendeza. Mfano: Suti aliyoinunua imemkaa vizuri.

Sentensi hii inazua dhana ya kumchukua vizuri na pengine kumfanya apendeze.

Maana nyingine za kitenzi hicho ni pamoja na kuweka makalio juu ya kitu; kuwa na nyumba au maskani mahali fulani; kuishi mahali kwa kipindi fulani; kushinda miongoni mwa nyingine nyingi.

Yumkini

Yamkini ile dhana ya mwonekano inavyojitokeza katika kitenzi kaa ndiyo huwafanya watu kudhani kuwa kinaweza kutumiwa katika ulinganishaji.

Uhalisia wa mambo hata hivyo ni kuwa ni kosa kukitumia kitenzi kaa kuonyesha mshabaha au mfanano uliopo baina ya vitu au watu.

Kitenzi hicho aidha hakipaswi kutumiwa mahali pa neno ‘kama’ ambalo hukusudiwa kuzua dhana ya shaka katika usemi.

Matumizi fasaha ya kitenzi hiki ni muhimu jinsi ulivyo ujumbe ambao watu hudhamiria kuuwasilisha.

You can share this post!

VYAMA VYA KISWAHILI: Chama cha Kiswahili katika Shule ya...

VITUKO: Mwinyi aamua kumwondoa fahali mmoja zizini,...

adminleo