• Nairobi
  • Last Updated March 18th, 2024 8:55 PM
VITUKO: Mwinyi aamua kumwondoa fahali mmoja zizini, Sindwele ndiye hasa!

VITUKO: Mwinyi aamua kumwondoa fahali mmoja zizini, Sindwele ndiye hasa!

Na SAMUEL SHIUNDU

MARA mbili sasa, Mwinyi alikuwa kapoteza kesi dhidi ya wadogo wake wa kazi waliotunduka.

Hali hii ilimchukiza si haba.

Aliziweka kesi hizi mbili kwenye mizani na akaona kwamba kesi ya mwalimu Pengo ilikuwa afadhali kwani alihamia shule ya kule Sidindi baada ya kumfedhehesha mbele ya halmashauri ya shule.

Kesi ya juzi iliyomhusisha Sindwele ndiyo iliyomkera zaidi. Sindwele alikuwa kamsukumia madai ya uongo na akasalia pale pale Maka.

Hali hii ilimkalia vibaya bwana Mwinyi, hangestahimili kuonana naye pale shuleni Maka kila asubuhi.

“Lazima mmoja wetu aondoke,” alijiambia kila alipomtia machoni.

“Haiwezekani fahali wawili wadumu katika zizi moja,” alijikariria.

Alipoliwazia hili la mafahali wawili katika zizi moja ndipo alipokumbuka ombi la bwana Sindwele miaka kadhaa iliyopita.

Wakati huo Sindwele alimbishia akitaka uhamisho. Alitaka kuhamishiwa Bushiangala karibu na ndege alilokuwa kaona.

Wakati huo, Sindwele alikuwa mwalimu mchapakazi na mwenye adabu kubwa. Mwinyi hangemwacha aende vivi hivi.

Akatumia ushawishi wake kulikanyagia ombi hili. Sasa alijutia hiki kitendo chake. Alihitaji kuutumia ushawishi uo huo kumwondoa Sindwele pale Maka.

Akainua simu kumpigia rafiki yake kwenye makao makuu ya huduma kwa walimu nchini.

“Mungu hamtupi mja wake!” ndivyo Sindwele alivyokiri baada ya kuupokea ujumbe wa uhamisho wake.

Alikumbuka mara ya kwanza alipoutaka uhamisho huu. Alikuwa ndipo mwanzo kamtia Sofia machoni.

Mshawasha

Enzi zile akiwa kijana akisumbuliwa na mshawasha wa kibethsheba. Akawa amwandama binti huyu wa Bushiangala.

Kwa vile alikuwa kama msasi aliyeishi mbali na windo lake, alipanga kuhamia kule mwituni Bushiangala kulikokuwa na windo lake.

Akatuma maombi ya kuhamia shule ya upili ya Bushiangala.

Alikuwa keshalisahau hili ombi la kutaka kuhamishiwa Bushiangala hasa baada ya kumwingiza Sofia chuoni. Lakini sasa Sofia mwenyewe kamwacha na kurejea kwa wazazi wake Bushiangala. Akawa ywahitaji kuanza ushawishi upya.

Juzi alikuwa kule na Pengo na wakweze wakamhakikishia kuwa Sofia wake angerejea, lakini sasa siku zinakuja na kwenda hajamwona huyo Sofia.

Alishuku kuwa wakwe zake walikuwa wanampangia jambo. Na hilo jambo walilolipanga halikuwa zuri. Mbona walimwongopa kwamba Sofia angerejea? Kwani walimchukuliaje?

Kama walifikiria kwamba angepoteza nauli za kila mara kusafiria hadi Bushiangala jinsi alivyofanya katika siku za uchumba wake na binti wao basi walikuwa wamekosea kwani alikuwa sasa kaipokea barua ya kuhamishiwa kuko huko Bushiangala.

Angekuwa karibu na wao ili abaini walichokuwa wakimpangia.

You can share this post!

NDIVYO SIVYO: Neno ‘kaa’ halipaswi kamwe...

MSHAIRI WETU: Sophy Onura ‘Johari Mwana Zawadi’

adminleo