Musila aanika 'ujanja' wa Kibaki dhidi ya Raila na Kalonzo
Na MWANDISHI WETU
MISUKOSUKO ya kisiasa iliyokumba muungano wa Narc, ilianza mara tu baada ya Rais Mstaafu Mwai Kibaki kuapishwa rais wa tatu wa Kenya mnamo Desemba 30, 2002.
Kulingana na mwafaka wa kisiasa katika muungano huo, Kamati Kuu ilitarajiwa kukutana mara tu baada ya kuapishwa kwa Mzee Kibaki, ili kuhakikisha kwamba umetekelezwa.
Kulingana na aliyekuwa mwenyekiti wa Chama cha Wiper, David Musila, kamati hiyo ilianza shughuli zake kwa kuwafahamisha viongozi wakuu wa kisiasa kuhusu wale waliopendekezwa kuteuliwa mawaziri.
Amerejelea haya kwenye wasifu wake mpya, Seasons of Hope (Nyakati za Matumaini), utakaozinduliwa rasmi Alhamisi hii.
“Chama cha LDP kilikuwa na orodha ya watu ambao kilitaka wateuliwe mawaziri na manaibu wao, ambayo iliwasilishwa kwa kamati hiyo. Wakati huo, hakukuwepo na tofauti yoyote katika chama chetu kuhusu orodha hiyo,” asema Bw Musila.
Anaeleza kwamba Mzee Kibaki alikuwa bado mgonjwa, hivyo hawakufahamu wale ambao wangependekezwa kuwa mawaziri kutoka mrengo wa National Alliance of Kenya (NAK).
Baadaye, mrengo wa LDP ulipendekeza kubuniwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu katika baraza la mawaziri, ambapo walimpendekeza Raila Odinga kupewa cheo hicho.
“Tulitarajia wenzetu katika NAK wangezingatia mwafaka huo, kwani ulikuwa umekubaliwa kwa nia nzuri kati ya pande hizo mbili. Tulishangaa sana wakati orodha ya LDP ilipowasilishwa kwa Mzee Kibaki lakini ikarudishwa kwetu,” asema Bw Musila.
“Rais alisema kwamba wajibu wa kufanya teuzi mbalimbali ni wake. Alikataa pendekezo la kubuniwa kwa nafasi ya Waziri Mkuu katika serikali yake,” akaeleza.
Hiyo ndiyo ilikuwa dalili ya kwanza kwamba hali haingekuwa shwari katika serikali hiyo, kwani baadhi ya makubaliano yalipuuzwa.
“Mbali na hayo, Bw Kibaki aliagiza pendekezo letu liwasilishwe kwake tu na Moody Awori, ambaye alikuwa mwenyekiti wa kamati hiyo. Tulikubali na kumpa Bw Awori orodha hiyo ili kumpa Kibaki,” anaeleza Bw Musila.
Viongozi wengi katika chama cha LDP walikuwa katika orodha hiyo. Miongoni mwao walikuwa Joab Omino kama mwenyekiti wa chama hicho na Bw Musila kama naibu mwenyekiti wake. Wengine ni: Raila Odinga, George Saitoti, Kalonzo Musyoka na Moody Awori.
Asema: “Hatukuwa na wasiwasi wowote kwamba Bw Kibaki angekosa kuzingatia makubaliano hayo, hadi siku alipotangaza baraza lake la mawaziri. Kwa mshangao wetu, Bw Kibaki alipuuza orodha yetu na kuwajumuisha watu ambao hawakushirikiana nasi kwenye kampeni za muungano huo. Walikuwa Linah Jebii Kilimo na Raphael Tuju. Watu pekee waliokuwa katika orodha hiyo tuliowapendekeza walikuwa ni Saitoti, Odinga, Awori na Kalonzo.”
Kulingana na Bw Musila, uteuzi huo ndio ulioanza mivutano iliyotokea baadaye na kuusambaratisha muungano huo.