• Nairobi
  • Last Updated March 28th, 2024 11:42 PM
Wakenya wanataka kuhamia majuu kusaka ajira – Ripoti

Wakenya wanataka kuhamia majuu kusaka ajira – Ripoti

Na LEONARD ONYANGO

WAKENYA zaidi ya thuluthi moja, wengi wao wakiwa wanaume, wanatamani kuhamia mataifa ya kigeni kwenda kusaka ajira.

Ripoti iliyotolewa na shirika linalotafiti masuala ya demokrasia, utawala na hali ya kiuchumi barani Afrika, Afrobarometer, inaonyesha kuwa asilimia 35 ya Wakenya wanatamani kuhamia mataifa ya kigeni kutokana na hali ngumu ya maisha humu nchini.

Sababu nyingine zinazowasukuma Wakenya kuhamia mataifa ya kigeni ni masomo, kutalii na kutafuta nafasi za kibiashara.

“Asilimia 65 ya Wakenya, haswa wazee wa kuanzia umri wa miaka 50 na zaidi hawatamani kuhamia nchi nyingine,” akasema mkurugenzi wa Afrobarometer Gyimah Boadi wakati wa uzinduzi wa ripoti hiyo jijini Nairobi.

Asilimia 40 ya wanaume wanatamani kuhamia nchi za kigeni kwenda kusaka ajira ikilinganishwa na asilimia 33 ya wanawake.

“Walio na hamu kubwa ya kuhamia nchi za kigeni ni kwenda kutafuta ajira ni vijana wa kati ya umri wa miaka 18 na 25. Zaidi ya nusu ya Wakenya walio na elimu ya vyuoni wanatamani kuhamia ughaibuni,” inasema ripoti ya utafiti huo uliofanywa katika mataifa 34 ya Afrika.

Asilimia 44 ya Wakenya walio na elimu ya sekondari pia wanaamini kuwa maisha yao huenda yakawa bora endapo watahamia nchi nyingine.

Jambo la kushangaza ni kwamba wengi wa Wakenya, asilimia 29, wanatamani kuhamia katika mataifa ya Jumuiya ya Afrika (EAC) kama vile Tanzania, Uganda, Rwanda, Burundi na Sudan Kusini.

Asilimia 27 wanatamani kuhamia mataifa ya Ulaya na Amerika (asilimia 22).

Ripoti inaonyesha kuwa zaidi ya nusu ya raia wa mataifa ya Cape Verde, Sierra Leone na Gambia wako tayari kuhamia nchi za kigeni kusaka ajira, kuepa machafuko na kuhepa umaskini.

Nchi ambazo raia wake wameridhika na hawatamani kuhamia nchi nyingine ni Madagascar, Tanzania na Mali mtawalia.

You can share this post!

Kituo cha kunyonyeshea watoto chazinduliwa

Ilinibidi nitoroke nisiuawe na mke wangu aridhi mali, asema...

adminleo