Ilinibidi nitoroke nisiuawe na mke wangu aridhi mali, asema profesa
NA BENSON MATHEKA
MHADHIRI na mtaalamu wa masuala ya maji, Profesa Edward Kairo, Jumanne alieleza mahakama kwamba, alilazimika kutoroka nyumbani kwake jijini Nairobi baada ya kupashwa habari kwamba, mkewe alipanga kumuua ili amiliki mali yake.
Profesa Kairo alisema aliamua kuacha nyumba yake ya kifahari mtaani Kileleshwa na gari ili kuokoa maisha yake baada ya kufahamishwa kwamba mkewe Mary Njoki Ndiba, ambaye kwa sasa wametengana, alikuwa amepanga njama ya kumuua.
“Nilipata habari za kuaminika kwamba mke wangu alikuwa akipanga kuniua ili amiliki nyumba yangu mtaani Kileleshwa, gari na ploti zangu mbili viungani mwa jiji la Nairobi. Niliamua kuhama nyumba yangu ili kuokoa maisha yangu,” aliambia Hakimu Mwandamizi wa Kibera Barabara Ojoo.
Mhadhiri huyo alikuwa akitoa ushahidi katika kesi ambapo Bi Njoki ambaye kwa sasa ni mwanachama wa bodi ya kudhibiti mashirika yasiyo ya kiserikali, ameshtakiwa kwa kughushi stakabadhi zake na kuhamisha umiliki wa gari lake.
“Nilimuachia gari hilo na nyumba lakini sikumpa idhini na sijawahi kumpa idhini ya kuhamisha umiliki wake,” alisema.
Bi Njoki amekanusha kwamba alighushi kitambulisho na sahihi ya Profesa Kairo ili kuhamisha umiliki wa gari hiyo aina ya Suzuki Escudo. Inadaiwa kwamba alitenda kosa hilo siku tofauti 2016. Alipoulizwa na wakili wa Bi Ndiba alipopata habari kuhusu njama za kumuua, Profesa Kairo alisema alipashwa na shemeji yake Bi Mary Njonjo.
“Mshtakiwa alizungumza na shemeji yangu Mary Njonjo na kumfahamisha kwamba alikuwa ameamua kunimaliza ili aweze kumiliki mali yangu. Niliamua kuchukua hatua za kuokoa maisha yangu,” alieleza. Alisema aliripoti kwa polisi na kuna kesi ya talaka katika Mahakama Kuu.
Hata hivyo, hakimu alisema kesi iliyokuwa mbele ya mahakama ilihusu kughushi stakabadhi na sio vitisho vya kuua. Profesa Kairo alisema alipoondoka kwake,aliacha ujumbe kumfahamisha Bi Njoki kwamba angemhamishia umiliki wa gari lakini akakanusha kwamba alijaza fomu na kumkabidhi.
Kesi itaendelea Julai 24.