Wabunge wazima uagizaji maziwa kutoka ng’ambo
Na CHARLES WASONGA
WABUNGE wameitaka Wizara ya Biashara kusitisha uagizaji wa maziwa kutoka nje, wakisema huawaathiri wafugaji wa ng’ombe wa maziwa kwa kupunguza mapato yao.
Wanachama hao wa kamati ya bunge kuhusu kilimo jana walisema haina haja kwa serikali kuendelea kuagiza bidhaa hiyo ilhali kiwango cha maziwa kinachozalishwa nchini kinatosheleza mahitaji ya soko.
“Kenya inazalisha kilo 5.7 bilioni kila mwaka ilhali hitaji la kitaifa ni kilo 5.2 bilioni pekee. Hii ina maana kuwa mwenendo wa serikali kuendelea kuagiza maziwa kutoka nje unawaumiza wakulima wetu na unapasa kukomeshwa mara moja,” akasema naibu mwenyekiti wa kamati hiyo ambaye pia ni Mbunge wa Navakholo, Emmanuel Wangwe.
Alisema uagizaji huo umechangia kupungua kwa bei ambayo wafugaji huuza maziwa yao kwa kampuni za kutayarisha maziwa kutoka Sh42 hadi Sh28 kwa lita moja.
“Katika hali hii, wakulima ndio wanaumia ikizingatiwa kuwa bei ya lishe ya mifugo ilipanda baada ya serikali kuanza kutoza bidhaa hiyo ushuru wa thamani ya ziada (VAT),” Bw Wangwe aliwaambia wanahabari katika majengo ya bunge, Nairobi.
Aliandamana na wenzake, Gabriel Kago (Githunguri), John Paul Mwirigi (Igembe Kusini), Justus Murunga (Matungu), Janet Sitienei (Turbo), Ferdinand Wanyonyi (Kwanza) na Silas Tiren (Moiben) na John Mutunga (Tigania Magharibi).
Wabunge hao walisema katika Januari pekee, wizara ya biashara iliagiza lita milioni 15 za maziwa ya maji na kilo 1.5 milioni ya maziwa ya unga.
“Hii ina maana kuwa, kufikia Desemba mwaka huu, Kenya itakuwa imeagiza zaidi ya lita 70 milioni ya maziwa ya maji na kilo 10 milioni ya maziwa ya unga. Hali hii itaua wafugaji wa ng’ombe wa maziwa na ndio maana Waziri Peter Munya anafaa kukomesha uagizaji huu mara moja,” akasema Bw Tiren.
Alisema uwepo wa maziwa mengi katika soko la humu nchini unafaidi kampuni kubwa za utayarishaji maziwa ambazo zimekuwa zikinunua maziwa kwa bei ya chini kutoka kwa wakulima huku zikitengeneza faidi kubwa.
“Tunataka kukinga wakulima dhidi ya unyanyasaji huu ambao sasa unaonekana kuendelezwa na serikali kupitia Wizara ya Biashara,” Bw Tiren alisema huku akifichua kuwa maziwa mengi huingizwa humu nchini hutoka Uganda.
Wabunge hao pia waliunga mkono hatua ya Bodi ya Maziwa Nchini (KDB) kusimamisha kwa muda utayarishaji wa sheria tata za kuongoza sekta hizo.
“Hatua hiyo ni nzuri kwa sababu sheria hizo ni dhalimu na zingewaumiza wakulima wadogo ambao humiliki ng’ombe wachache wa maziwa. Tunaitaka KDB kuhakikisha imeandaa mazungumzo na wadau wote katika sekta hii kabla ya kuchapisha sheria hizo,” akasema Bw Wangwe.