MWANAMUME KAMILI: Nyie mnaotangazia umma ya chumbani ni gumegume
Na DKT CHARLES OBENE
VITA vya wapendanao mitandaoni fedheha kwa jamaa na jamii.
Lau tungekuwa wenye akili timamu, tungekoma usabasi mitandaoni!
Sijapendezwa wala sioni uwezekano kufurahia utoto wa watu wazima kupakana tope kwenye mitandao ya kijamii.
Sote tunakubaliana kwamba afadhali mume anayesema yaliyomkwaza moyoni kuliko baadhi ya malofa wenye mazoea kununa na kufumba hasira kwa miezi ama miaka.
Usununu sio tabia ya mwanamume kamili.
Tatizo ni kwamba kuna sampuli ya wanaume kwa wanawake wasiojua lipi la kusema hadharani.
Yaani wanaweza ibuka na tope na kumfedhehi mwenza kwa njia inayodunisha mno!
Huo sio ubinadamu unaostahiki mja wa karne hii.
Si tukizi kusoma habari mitandaoni ama magazetini jinsi mapenzi yalivyogeuka na kuwa uwanja wa fedheha.
Nini hasa humchochea binadamu hadi kumshawishi kuvunja heshima katika husiano? Iweje mtu akaona heri kutundika picha za uchi mitandaoni? Kweli, heri mende na akili zake ndogo.
Nyanja
Mitandao ya kijamii ndio kwanza nyanja za kupakana tope wanazotumia mahasidi na wenye kinyongo!
Wiki jana, mwanamume mmoja aliona heri kuchapisha habari na kuzianika siri za familia mtandaoni. Kwa hamaki za mkizi, gumegume yule alimwaga mtama kwenye kuku wengi na kumwacha mpenziwe kachutama, tena mwingi wa soni.
Bila shaka kidosho yule aliona aibu kufuatia picha zake za utu uzima kutundikwa hadharani mitandaoni.
Ajabu ni kwamba mke mhusika alijibu fedheha ile kwa namna iliyoshangaza hata zaidi. Hakuficha chochote kilichostahili kufichwa baina yao.
Bila shaka mume yule alijutia uamuzi wake. Inadaiwa kwamba mahasidi wenyewe walikuwa wamekwisha achana miaka saba iliyopita.
Swali zito ni kwamba iweje vita vya mitandaoni kuzuka hata baada ya kila mmoja kwenda njia yake? Kulikuwa na haja gani kufedheheshana mitandaoni?
Mbona watu wazima walishindwa kuyakumbuka mema baina yao wakaweka hasira mbele? Jamani wangwana, hebu tuuacheni ujahili na utoto wa kuvunjiana heshima mitandaoni.
Ubinadamu ni kudumisha mshikamano huku kila mmoja akijitahidi kujiepusha na hawaa za nafsi sisemi uchu wa kutiliana doa. Hiyo ndiyo tajriba ya mwanamume kamili.
Kinyume na matarajio ya wangwana; tunaishi miongoni mwa wanadamu wanaopapurana na kulumbana kila uchao kama fisi wanaong’ang’ania mzoga! Kisa na maana? Mwanamume wa leo mwingi wa usununu na dhiki moyoni. Hafukuliki wala hafungui roho kinyaa kikamwondokea.
Mtu kutojieleza
Wanawake nao ni hamira kuche kusiche.
Kuishi na mwanadamu asiyejieleza waziwazi ni sawa na kula kitoweo kilichotonewa sumu. Japo chakula hiki kinaweza kuwa kitamu kwa ukolevu wa virutubisho vyake, lakini mwishowe madhara yake ni mauti.
Hivyo ndivyo alivyo mwanamume asiyejua kunena na kujiondolea fundo moyoni. Anaweza kukutia wazimu kabla ya msimu wa kichaa. Tahadharini nyie vimwana mnaopenda kupendwa!
Tatizo kubwa linalosibu maisha ya wanadamu wa leo ni uhasama na uadui unaotokana na udhanifu wa mwanamume wa leo. Hivi tulivyodhikika maishani, nani mwenye moyo wa jiwe asiyetaka mpenzi mwingi wa ucheshi, umbuji, unyofu na ucha?
Lakini wapi? Baadhi ya wanaume wa leo wana fundo moyoni wala hawana haja kujieleza. Mume sampuli hii ni moto wa kuotea mbali!
Upenyenye na upeketevu wa wanaume wa leo umekuwa ufa unaoporomosha misingi thabiti ya uchumba na uchu wa mahaba.
Hawajui mzaha au ucheshi hawa wanaume wanunaji! Dunia yenyewe ni mawe. Mke yupi anayetaka kuishi na jiwe nyumbani?
Na sio unyamavu wa wanaume tu unaochusha maisha ya vimwana wa leo. Wako gumegume wanaopeleka matatizo ya nyumbani au chumbani na kuyaweka mikekani, akina yakhe kuyajadili na kuyatafuna katika mahakama ya malofa wasiojua kitu ila kuchana majani vibarazani! Hawajui umuhimu wa wanandoa kupigana kumbo chumbani na kuwapa umma miale ya tabasamu tu. Nani atajua kwamba chumbani mlikuwa na moshi?
Vijimambo vidogovidogo vya kutulizwa zuliani havina haja kumwagwa kwenye kuku wengi mitandaoni. Isitoshe, mwanamume kamili mwingi wa hekima! Anajua vipi kutunza heshima na kujenga jina. Nyie mnaotangazia umma ya chumbani ni gumegume.
Hakuna haja kujifanya wanaume kamili!