Jombi atoroka mke aliyeletewa na mamake
NA LEAH MAKENA
KANGETA, MAUA
Kalameni wa hapa alilazimika kutoroka nyumbani kuhepa mwanadada aliyechaguliwa na mama yake kuwa mke wake.
Jamaa alikataa kata kata kukubali mwanadada aliyechaguliwa na wazazi wake na walipomshinikiza akaamua kutoroka na kurudi mjini alikokuwa akiishi baada ya kumaliza masomo.
Kwa zaidi ya miaka minne, polo alikuwa chuoni kusoma licha ya wazazi kumtaka kuoa wakidai umri wake ulikuwa umesonga. Alitia masikio nta na kubukua hadi akahitimu ndipo akafika nyumbani kutoa shukrani kwa wazazi.
Hakuamini alipofika nyumbani kwani alifanyiwa kikao na wazee na kutakiwa kumpokea mwanadada aliyekuwa katika nyumba yake kuwa mkewe.
Penyenye zinasema jamaa hakutakiwa kupinga uamuzi wa wazazi wake wa kumchagulia mke.
“Kama unavyojua, imekuwa desturi ya vijana kutafutiwa wachumba kwani tunajua msichana anayekufaa zaidi kama wazazi. Tushalipa mahari na tunachotaka ni wewe kumpokea kama mke wako ili muendeleze kizazi chetu,” wazee walimshauri.
Yasemekana jamaa alikataa akisema alikuwa na mchumba na walikuwa wakipanga harusi.
“Mimi nishapata mpenzi na tunataka kuanza mipango ya harusi punde tu baada ya kupata ajira. Enzi za kutafutiwa wachumba zilipita, naomba mniruhusu nifanye maamuzi yangu binafsi,” kijana alijitetea.
Hata hivyo hakuweza kuwashawishi wazee kubadilisha nia kwani walisisistiza kuwa hawangekubali msichana wa mbali wasiyejua tabia zake.
Hapo ndipo jamaa alikubali agizo lao shingo upande kwa lengo la kuwafurahisha kwa muda. Inasemekana kuwa jioni hiyo, jamaa alitoka bila kuaga na kuishia mjini ambako aliendeleza mipango ya harusi na mpenzi wake bila kufahamisha wazazi.
Vitisho vya wazee kwamba wangemlaani havikumshtua na mwanadada aliyechaguliwa akalazimika kurudi kwao kujaribu bahati kwingine.