• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 6:55 AM
Barclays yaamriwa ilipe serikali magari iliyonunulia kampuni za kujenga mabwawa

Barclays yaamriwa ilipe serikali magari iliyonunulia kampuni za kujenga mabwawa

Na RICHARD MUNGUTI

MAHAKAMA Kuu Jumatatu iliiamuru Benki ya Barclays ikabidhi afisi ya Mkurugenzi wa Jinai (DCI) magari iliyonunulia kampuni ya Italia iliyopewa kandarasi ya kujenga mabwawa ya Aror na Kimwarer na kupelekea serikali kupoteza zaidi ya Sh20 bilioni.

Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma (DPP) Noordin Haji naye aliomba mahakama kuu imruhusu ajiunge na kesi iliyowasilishwa na benki ya Barclays kuhusu miradi hiyo.

DPP amesema kampuni 122 zilipokea Sh500 milioni kutoka kwa Benki ya Barclays tawi la Waiyaki Way.

Kampuni ya Italia CMC Di Raveva Itenera Jv Kenya, iliyopekea pesa hizo ilikuwa inalipwa kwa  Dola za Marekani, Euro na Shilingi za Kenya.

Mahakama iliaelezwa ujenzi wa mabwawa haya umesababisha mikwaruzano mikali kati ya maafisa wakuu serikalini huku miito ikitolewa wanaohusika watiwe nguvuni na kushtakiwa.

Majimbizano yamekuwa yakisheheni kati ya Naibu Rais Dkt William Ruto na baadhi ya wanasiasa kutoka kwa mrengo wa Jubilee.

Benki ya Barclays iliwasilisha ombi mbele ya Jaji Francis Tuiyot ikiomba mwongozo utolewe kuhusu magari yaliyonunuliwa na pesa ilizopokea.

Akiwasilisha ombi la DPP, naibu wa mkurugenzi Bw Alexander Muteti alisema itakuwa hasara kuu kwa umma iwapo ombi hilo halitakubaliwa.

Jaji Tuiyot aliamuru isikizwe mnamo Mei 21 mwaka huu ndipo DPP awasilishe ushahidi jinsi mabilioni ya pesa yalivyotoweka katika akaunti za kampuni na watu binafsi.

Afisa anayechunguza kashfa hiyo ya Sh65 bilioni Inspekta Gilbert Kitalala amesema ripoti aliyopokea sasa imebaini Mamlaka ya Kustawisha Bonde la Kerio (KVDA) ilipunja fedha hizo.

Naibu wa Mkurugenzi wa Mashtaka ya Umma Alexander Muteti alimweleza Jaji Francis Tuiyot kuwa iwapo DPP hataunganishwa katika kesi hiyo mambo kadha yataenda kombo.

Bw Muteti alieleza mahakama kuwa Insp Kitalala anayechunguza kesi hiyo amepokea taarifa za kina jinsi mabilioni ya pesa yalipunjwa na kufikia sasa “Sh20.5bilioni zimelipwa kampuni na bado ujenzi wa mabwawa haujaanza.”

“Kwa ajili ya bwawa la Aror kampuni hiyo ya CMC Di Ravena Itenera JN ilipokewa sehemu ya malipo Sh4.3 bilioni na kwa niaba ya Kimwarer ilipokea Sh3.4bilioni,” akasema Insp Kitalala.

Uchunguzi umebaini kuwa kampuni ya Toyota Kenya ilipokea Sh160,275,928 kwa kuuza magari 45 miundo ya Prado, Fortuner, Corolla, Hiace na lori ndogo za Double Cabin.

Kati ya magari haya 45, 17 yaliandikishwa kwa jina la CMC Di Ravena Itenera JN Kenya na tisa kati ya haya yanazuiliwa katika afisi ya DCI.

Kufikia sasa magari 37 yamebambwa na kuzuiliwa katika afisi ya DCI ya Nakuru. Kesi itaendelea Mei 21.

You can share this post!

GSU yajikwaa Prisons ikitamba voliboli ya Klabu Bingwa...

MAPOZI: Dr King’ori

adminleo