• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 8:55 AM
AUNTY POLLY: Nakwepa mitandao ya kijamii kama Ukoma

AUNTY POLLY: Nakwepa mitandao ya kijamii kama Ukoma

Na PAULINE ONGAJI

KWA wiki mbili sasa nimeepuka mitandao ya kijamii kutokana na matusi ambayo nimekuwa nikipokea. Kinachoshangaza hata zaidi ni kwamba matusi haya yanatoka kwa marafiki zangu wa zamani; watu ambao wakati mmoja niliwaamini sana na hata kuwaeleza mambo yangu ya siri. Nimejaribu kuhusisha walimu wangu katika suala hili lakini ni kana kwamba hawana haja ya kunisaidia. Naogopa kuwaeleza wazazi wangu kwa sababu hawafahamu iwapo nina akaunti yoyote ya mtandao wa kijamii. Nifanyeje?

Yasmine, 15, Mombasa

Kwanza kabisa hongera kwa kujitokeza na kuzungumzia suala kama hili. Ningependa kukujulisha kwamba ni vyema kuwajulisha wazazi wako kuhusu unachopitia badala ya kukimya. Afadhali wakusute na tatizo lisuluhishwe. Hii ni kwa sababu dhuluma za aina hiyo huchangia pakubwa visa vya vijana umri wako kujitia kutanzi. Pia, unaweza jaribu kuzungumza na mtu yeyote mkomavu ambaye ataelewa hali yako. Yaweza kuwa mwalimu, jamaa au mshauri nasaha shuleni. Ni vyema kwamba umeamua kukaa mbali na mtandao wa kijamii na ningependa kukushauri uzidi kufanya hivyo. Badala yake unaweza kujihusisha na mambo mengine ambayo yataelekeza mawazo yako kwingineko kama vile kuweka shajara kueleza hisia zako, kusikiza muziki, kutazama filamu, kujihusisha na spoti au kujumuika na watu wengine. Pia, unapaswa kufahamu kwamba kuna sheria zinazolinda watu kutokana na dhuluma mtandaoni, na hivyo unaweza kumchukulia hatua yeyote anayekiuka haki yako kwa njia hii.

 

Mpenzi wangu wa zamani ananitumia jumbe kila mara akinisihi turudiane lakini mimi simtaki. Anasisitiza sana kiasi kuwa nimekuwa nikiwazia ‘kublock’ simu zake. Nifanyeje?

Caroline, 18, Nairobi

Ni kawaida kuwa na hisia za aina hii baada ya kuachana na mtu mliyekuwa naye katika uhusiano. Hata hivyo swali langu ni kwa nini mliachana? Je, umemweleza kwamba hautaki kurudiana naye? Ikiwa umemweleza na awali alikuwa anakupenda kwa dhati, basi anapaswa kuheshimu uamuzi wako. Zaidi ya yote unapaswa kufahamu kwamba kukatika kwa uhusiano hakumaanishi mwisho wa mawasiliano hasa ikiwa nyote mumekubaliana na uamuzi wa kuachana na bado mnadumisha urafiki.

You can share this post!

MAPOZI: Dr King’ori

SWAGG: Bradley Cooper

adminleo