• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 8:55 PM
Afisi ya Rais wa Algeria yatangaza atajiuzulu Aprili 28

Afisi ya Rais wa Algeria yatangaza atajiuzulu Aprili 28

Na MASHIRIKA

AFISI ya Rais Abdelaziz Bouteflika wa Algeria imetangaza kwamba ataachia madaraka Aprili 28 kabla ya kutamatika muda wake.

Tangazo hilo lilikuja akiwa tayari amebuni serikali ya mpito huku shinikizo zikiongezeka kumtaka ang’atue uongozini.

Bouteflika amechukua hatua hiyo baada ya Mkuu wa Jeshi, Ahmed Salah kuongeza mwito wa kutaka mageuzi ya kikatiba ili kumwondoa mamlakani.

Ripoti pia ziliibuka kwamba huenda akajiuzulu kabla ya uchaguzi mkuu.

Kwenye taarifa iliyotolewa na afisi yake, rais huyo alimteua Sabri Boukadoum kuwa waziri mpya wa masuala ya kigeni, kuchukua mahali pa Ramtane Lamamra, aliyechukua nafasi hiyo mapema Machi.

Wengine waliobadilishwa kwenye mageuzi hayo ni Gavana wa Benki Kuu Mohamed Loukal aliyeteuliwa kuwa waziri wa fedha, huku Mohamed Arkab akiteuliwa waziri wa kawi.

Baraza jipya la mawaziri linaongozwa na Waziri Mkuu, Noureddine Bedoui, aliyeanza kuhudumu mnamo Machi 11.

Waandamanaji wamekuwa wakimshinikiza Bouteflika kung’atuka pamoja na washirika wake wote wa kisiasa.

Maandamano hayo yalianza mnamo Februari baada ya rais huyo kutangaza kuwa atawania urais kwa kipindi cha tano kwenye uchaguzi uliopangiwa kufanyika mwishoni mwa Aprili.

Rais huyo mkongwe ana umri wa miaka 82 na anaugua kiharusi.

Bouteflika alitangaza kujiondoa kama mwaniaji wa uchaguzi huo, lakini akauchelewesha, akishikilia kuwa atajiuzulu tu baada ya katiba kubadilishwa na mrithi wake kuchaguliwa.

Viongozi wa upinzani hata hivyo walikashifu hatua hiyo, wakiitaja kama njama ya kuongeza muda wake uongozini, unaotarajiwa kukamilika rasmi mnamo Aprili 28.

Kiongozi huyo alianza kuugua mnamo 2013 baada ya kupatwa na kiharusi. Katika siku za hivi majuzi, amejipata pabaya, kwani hata washirika wake wa karibu wa kisiasa wamemgeuka, wakiunga mkono shinikizo za kumtaka kuondoka uongozini.

Jeshi pia limetangaza kuunga mkono miito ya kumtaka ang’atuke, likitaja afya yake kama kizingiti kikuu.

“Hali ya afya ya rais inaendelea kudorora. Wakati umefikawakati azingatie miito ya waandamanaji wanaomtaka aondoke ili kutoa nafasi kwa uongozi mpya,” akasema Jenerali Salah.

Akaongeza: “Lazima tubuni suluhisho litakalotusaidia sisi sote na litakalozingatia kanuni zote za kikatiba.”

Utawala mpya

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa (UN), Antonio Guterres pia ameunga mkono juhudi za kubuni utawala mpya nchini humo bila umwagikaji damu.

Akihutubu katika Kongamano Maalumu la Nchi za Kiarabu mnamo Jumapili nchini Tunisia, Guterres alisema kuwa pande zote husika zinapaswa kubuni utaratibu wa serikali mpya bila ghasia, ambazo huenda zikasababisha maafa.

“Tunaunga mkono juhudi zozote ambazo zitahakikisha uwepo wa utawala mpya bila mzozo wowote wa kisiasa,” akasema.

Bouteflika alirejea Algeria majuma kadhaa yaliyopita baada ya kukaa kwa karibu mwezi mmoja nchini Uswizi akipokea matibabu.

You can share this post!

SWAGG: Bradley Cooper

SHANGAZI AKUJIBU: Mpenzi wa kando hukasirika nikimpigia...

adminleo