• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 2:16 PM
Ni muhimu kujiandaa kupanda miche ya miti mvua ikibisha hodi

Ni muhimu kujiandaa kupanda miche ya miti mvua ikibisha hodi

Na SAMMY WAWERU

WIZARA ya Mazingira imekuwa katika harakati za kuhamasisha kampeni ya upanzi wa miti ili kuafikia kigezo cha asilimia 10 ya misitu nchini ifikapo 2022.

Shughuli hii ilianza mwaka 2018 chini ya uongozi wa Waziri Keriako Tobiko na wadau husika.

Bajeti ya Sh18 bilioni iliandaliwa ili kufanikisha upanzi wa miti kwa muda wa miaka mitano ijayo, Rais akawasilishiwa kwa minajili ya ufadhili.

Machi 2018 akizungumza katika hafla ya upanzi wa miti Msitu wa Ngong, Bw Tobiko alisema wizara yake itashirikiana na wadau wote kufanikisha uhifadhi wa mazingira.

“Tunahimiza Wakenya wote kushiriki kikamilifu katika zoezi hili, ili kuimarisha hali ya mazingira nchini,” waziri Tobiko alihimiza.

Hamasisho hilo lilijiri baada ya mito mingi mikuu nchini kukauka, hivyo kuathiri masuala muhimu kama uhai wa wanyamapori.

Kwa mfano, kukauka kwa Mto Mara kulitajwa kuathiri uhamaji wa kongoni kutoka mbuga ya Masai Mara hadi Serengeti nchini Tanzania.

Kulingana na Shirika la Umoja wa Mataifa kuhusu mazingira (UNEP), kiwango cha misitu nchini kimepungua kutoka asilimia 10 katika miaka ya themanini hadi asilimia 1.7 pekee kufikia 2015.

Umoja wa Mataifa (UN) kwenye ripoti yake ya mwaka 2017 ilisema inalenga kupanda miti kwenye misitu hekta milioni 120 kote duniani, katika malengo yake ya ruwaza ya 2030.

Ukame na njaa inayoshuhudiwa nchini kwa kiasi fulani vyote vinahusishwa na ukataji wa miti. Misitu ndiyo vyanzo vya maji hasa mito, na inapoharibiwa ina maana kuwa ukame utajiri.

Aidha, miti inaaminika kuwa kivuto cha mvua.

Itadara ya utabiri wa hali ya hewa inasema kufikia huu mwezi Aprili, huenda taifa likaanza kupokea mvua katika maeneo mengi, na wataalamu wa masuala ya ustawi wa misitu wanashauri huu ndiyo muda muafaka kujiandaa kupanda miche.

Kulingana na Bw Kiruthi Junior, mtaalamu wa miti na kilimo, serikali inapaswa kukaza kamba hamasisho la upanzi wa miti mvua inapobisha hodi ili kusaidia kuhifadhi misitu.

“Kampeni isiwe wakati taifa linakumbwa na majanga ya ukame na mito kukauka. Ikiwezekana ifadhili wananchi kwa miche,” anashauri mdau huyu.

Anaongeza kusema kuwa Kenya ina mashamba makubwa ya umma na kibinafsi, yasiyopandwa chochote na kwamba sehemu fulani inapaswa kugeuzwa kuwa misitu ili kuafikia malengo ya uhifadhi wa mazingira. “Kigezo cha kupata asilimia 10 ya misitu ifikapo 2022 itaafikiwa serikali ikihimiza wananchi wapande miti msimu huu mvua inakaribia kunyea,” anasema Bw Kiruthi.

Kulingana na Richard Maina, mkulima wa miche Nyeri, kila mwananchi anafaa kujitolea mhanga kuvalia njuga suala zima la uhifadhi wa mazingira. Mwanamazingira huyu anahoji miti iwe kipenzi cha kila mmoja ili kunusuru vyanzo vya maji.

Richard Maina, mkulima wa miche ya miti Nyeri wakati wa mahojiano. Picha/ Sammy Waweru

 

“Bila mapenzi ya mazingira hutaweza kuyahifadhi. Tupende nchi yetu kwa kupanda miche kwa wingi, hasa msimu wa mvua,” afafanua Bw Maina.

Shinikizo lake kuanza upanzi wa miche lilitokana baada ya kuona Mto Chania, unaopitia pembezoni mwa mji wa Nyeri unakauka kwa sababu ya uhabirifu wa Msitu Aberdare, ambao ndio chanzo chake cha maji. Kiwango cha samaki waliokuwemo awali pia kimepungua.

“Mto huu haupiti kimo cha maji futi moja, ilhali awali mvua ingenyea yalikuwa zaidi ya futi nne. Uharibifu wa Msitu Aberdare umeuathiri kwa kiasi kikubwa,” akalalamika wakati wa mahojiano na Taifa Leo.

Maina alianza upanzi wa miche 2001, na anahimiza serikali, mashirika yasiyo ya kiserikali na watu binafsi kutilia mkazo upandaji wa miti ili kuhifadhi mazingira, yanayoonekana kuwa katika hatari kushambuliwa na wahuni. “Kampeni kali ya upanzi wa miti ifanywe, la sivyo taifa hili litaishia kuwa jangwa,” aonya.

Marufuku ya ukataji wa miti katika misitu ya umma, iliyotolewa 2018 ni ya hadi Novemba 24, 2019. Serikali iliitangaza kwa sababu ya kilio cha umma kwa uharibifu wa misitu.

You can share this post!

MAPISHI: Ugali na sukumawiki

WAKILISHA: Asambaza teknolojia mashinani

adminleo