• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 4:25 PM
WAKILISHA: Asambaza teknolojia mashinani

WAKILISHA: Asambaza teknolojia mashinani

Na PAULINE ONGAJI

AMEJITWIKA jukumu la kuhakikisha kwamba watoto na vijana katika sehemu za mashambani wanafikia teknolojia ya kisasa kama mbinu ya kuwasaidia kwenda sambamba na sehemu zingine duniani.

Kutana na Caleb Ndaka, mwanzilishi mshirika wa Kids Comp Camp, mradi unaonuia kusaidia watoto na hata watu waliokomaa hasa katika maeneo ya mashambani kufikia viwango vya kisasa vya kiteknolojia.

Ni mradi ambao kwa kipindi cha takriban miaka mitano umehudumia zaidi ya wanafunzi 8,000 kati ya miaka minane na 18 nchini Kenya na Rwanda.

“Hapa nchini tumepeleka mafunzo yetu katika shule za msingi za Masii Township, Muhoroni Oduwo, Madogo Adhama, Kabuku na Kawangware Chosen Children of Promise miongoni mwa zingine,” aeleza.

Mradi huu unahusisha kutoa mafunzo ya kompyuta na mtandao kwa watoto, vijana na hata watu waliokomaa.

“Kwa kawaida tunachukua muda nao na kutafiti kuhusu matatizo makubwa yanayowakumba kabla ya kubaini jinsi ya kutoa mafunzo yetu. Kisha tunashirikiana na taasisi zilizo karibu kuanzisha mafunzo kwa watoto hasa baada ya shule,” aeleza.

Pia wamekuwa wakihusisha vijana, wazazi na walimu katika mafunzo haya.

“Tuligundua kwamba zaidi ya 90% ya watu tuliokumbana nao katika harakati hizi, walikuwa wanajifunza komputa kwa mara ya kwanza,” asema huku akiongeza kuwa hii ilichochea uamuzi wao kuzama zaidi katika mradi huu.

Msukumo huu umewafanya kuteua na kufunza zaidi ya wahudumu 1,000 wa kujitolea, wakufunzi wa kijamiii na wahitimu wapya kutoka zaidi ya vyuo vikuu kumi kusaidia katika mradi huu.

Pia, wameshirikiana na mashirika makuu kama vile General Electric (GE), Microsoft, Dimension Data na Cloud Factory kutoa huduma ya kijamii, vilevile kuwashawishi kukubali wafanyakazi wao kuja kutoa mafunzo haya.

Na ufanisi wao katika kipindi cha takriban miaka mitano iliyopita unaonekana kwani wamehudumia zaidi ya watu 20,000 Afrika Mashariki.

“Kama mbinu ya kuunda rasilimali za kuendeleza shughuli zetu, tunawatoza watu wazima ada kidogo ili kupata huduma hii. Pesa tunazopokea husaidia kutoa mafunzo kwa watoto katika maeneo ya mbali bila malipo,” aeleza.

Msukumo wa kuanzisha mradi huu ulianza mwaka 2014 wakati huo akiwa katika mwaka wake wa mwisho katika Chuo Kikuu cha Kilimo na Teknolojia cha Jomo Kenyatta (JKUAT).

“Nilikuwa nakaribia kumaliza masomo ya Teknolojia ya Mawasiliano (IT) ambapo pamoja na marafiki zangu tulikuwa na mazoea ya kuzuru sehemu za mbali kujivinjari,” asema.

Wakati mmoja wakiwa wanarejea kutoka kwa mojawapo ya ziara zao, walianza kujadiliana kuhusu jinsi ambavyo wangechangia katika kuleta mabadiliko katika jamii hasa kupitia wanachojifunza chuoni.

Kuzuru

Wazo lao la kwanza asema lilikuwa kuzuru shule fulani kijijini ambayo haikuwa hata na mafunzo sahili ya kompyuta.

“Katika darasa moja nakumbuka tulipata kwamba ni watoto watatu pekee kati ya 60 ambao walikuwa wamewahi kuona kompyuta,” aeleza huku akiongeza kwamba ni hapa walikata kauli kuanzisha mradi huu.

Mradi huu umeenda hatua zaidi kwa kuimarisha maisha ya jamii ambazo watoto hawa wanatoka. Wanafanya hivi kwa kuwasaidia kujikuza kiuchumi kupitia mtandao na simu za kisasa.

“Tuligundua kwamba asilimia 40 ya wazazi ambao watoto wao wamehudhuria mafunzo katika vikao vyetu wanamiliki biashara ndogondogo ambazo kama zingine katika maeneo ya mashambani, hazidumu kutokana na sababu mbalimbali,” aeleza.

Hivyo wananuia kuwapa ufadhili wa mafunzo ya kiteknolojia vijana wanaotoka katika familia maskini.

“Tunanuia kutoa nafasi 25 za ufadhili, kila moja ya thamani ya Sh5,000 kusaidia vijana 25 kupata mafunzo katika masuala ya kiteknolojia kama vile kuunda wavuti na matangazo kupitia video miongoni mwa mengine kama mbinu ya kujipa kipato,” aeleza.

Tunafanya hivi kwani tunaelewa kwamba biashara ndogo zikishamiri, jamii zitaimarika na zitakuwa na uwezo wa kusaidia watoto wao.

You can share this post!

Ni muhimu kujiandaa kupanda miche ya miti mvua ikibisha hodi

Madai ya visa vya ubakaji yaongezeka Gatundu Kaskazini

adminleo