• Nairobi
  • Last Updated March 29th, 2024 7:50 AM
UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sera ya lugha ya kufundishia katika mataifa ya Afrika

UKUMBI WA LUGHA NA FASIHI: Sera ya lugha ya kufundishia katika mataifa ya Afrika

Na MARY WANGARI

NCHINI Msumbiji, lugha ya kufundishia inayotumika ni Kireno, ingawa marekebisho ya Katiba ya taifa hilo ya mwaka 1990 yanasisitiza kuwa lugha ya taifa iwe lugha ya wenyeji (Kibantu).

Kamwendo (2000) anasema kwamba sera ya lugha ya kufundishia nchini Malawi ni Kiingereza ingawa Chichewa ndiyo lugha ya taifa inayozungumzwa na asilimia hamsini ya wananchi.

Lengo la elimu kwa wote halina maana ikiwa mazingira ya lugha ya kufundishia hayatafanikiwa jinsi anavvoeleza Brock-Utne (2005).

Ni kwa mantiki hii ambapo tunabaini kuwepo  umuhimu mkubwa kwa nchi za kiafrika kufumbua macho kwa kuthamini lugha zao ili zitumike kufundishia katika viwango vyote vya elimu (Brock-Utne, 2005).

Kwa mujibu wa Mekacha (2000), Sera ya lugha nchini Tanzania ni matamko na maagizo ya viongozi yasiyoandikwa, yanayoagiza lugha ipi itumike au isitumike katika baadhi ya maeneo rasmi ya matumizi ya lugha.

Kulingana na sera ya Elimu na mafunzo (2014), Kiingereza na Kiswahili ni lugha zinazotumika kwa kufundishia na kujifunzia katika ngazi mbalimbali za elimu na mafunzo.

Isitoshe, Tume ya Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania (1980), ilipendekeza kwamba Wizara ya Elimu kwa kutumia vyombo vyake, Taasisi ya Ukuzaji wa mitaala, vyuo vikuu kwa ushirikiano na Baraza la Kiswahili la Taifa, ibuni mikakati kabambe ya kuwezesha shule na vyuo vyote nchini kufundisha masomo yote kwa kutumia Kiswahili kuanzia kidato cha kwanza ifikapo Januari 1985 na Chuo Kikuu kuanzia 1992.

Hatahivyo, ni jambo la kutamausha kwamba pendekezo hilo halikutekelezwa na badala yake mnamo 1984, serikali ilitoa tamko linalosisitiza na kuimarisha lugha ya Kiingereza kama lugha ya kufundishia elimu ya juu.

 Sera ya elimu na mafunzo  (1995) ilielekeza kuwa lugha ya kufundishia na kutolea mafunzo ya sekondari itakuwa Kiingreza. Serikali ilitoa Sera ya Utamaduni iliyodoekeza kuhusu mpango maalum wa kuwezesha elimu na mafunzo katika ngazi zote kutolewa katika lugha ya Kiswahili.

Inavunja moyo kwamba sera hiyo haitaji ni lini uamuzi huu utaanza kutekelezwa wala hatua za maandalizi ya utekelezaji wake.

 

Baruapepe ya mwandishi: [email protected]

Marejeo

Bryman A. (2008). Social Research Methods. London: Oxford University Press.

Cummins, J. (2008). Teaching for transfer. Challenging the two solitudes assumption in Bilingual education.In J. Cummins & N.H Homberger (Eds),Encyclopedia of Language and Education,2nd Edition,Volume 5.New York:Supringer Science + Business Media LLC.

Enon C.J. (1995). Educational Research, Statistics and Measurement. Kampala: Makerere University.

You can share this post!

AFYA: Kitunguu saumu kina faida zozote kiafya?

MAPISHI: Matoke na nyama ya ng’ombe

adminleo