Michezo

GSU yapata ushindi wa kwanza voliboli ya Afrika

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na GEOFFREY ANENE

MABINGWA wa Kenya, GSU, hatimaye wamepata ushindi wao wa kwanza katika mashindano ya Klabu Bingwa ya Voliboli ya Afrika yaliyoingia siku ya tatu Jumatano jijini Cairo nchini Misri baada ya kubwaga AS Fag kutoka Guinea kwa seti 3-0.

Vijana wa kocha Gideon Tarus waliingia mchuano huu wa Kundi D wakiwa na presha sana baada ya kupepetwa seti 3-2 dhidi ya Assaria mnamo Aprili 1 na kupokea dozi sawa na hiyo Aprili 2 dhidi ya Nemo Stars ya Uganda.

Washindi hawa wa medali ya shaba mwaka 2005 walifufua matumaini finyu ya kuingia robo-fainali kwa kulemea Fag kwa alama 25-13, 25-12 na 25-14.

Mabingwa wa zamani wa Kenya, Prisons watalimana na miamba wa Cameroon, FAP saa mbili usiku Jumatano wakihitaji ushindi ili kufufua ndoto ya kutinga mduara wa nane-bora baada ya kupoteza mechi ya pili ya Kundi C dhidi ya miamba wa Libya, Swehly 3-1 Aprili 2.

Vijana wa David Lung’aho walianza vyema dhidi ya Swehly kwa kuishinda katika seti ya kwanza 25-22, lakini wakazidiwa maarifa 25-19, 25-19, 29-27 katika seti tatu zilizofuata.

Prisons, ambayo ilinyakua medali ya fedha mwaka 2011, iliingia mechi ya Swehly na motisha ya kuchapa Wolaita ya Ethiopia 3-0 Jumatatu.

GSU na Prisons ziliapa kabla ya mashindano kuanza Aprili 1 kupigania taji vilivyo. Dalili zinaonyesha zitahitaji kufanya kazi ya ziada katika makundi yao kwanza. Timu 22 zhmekusanyika Cairo kwa makala ya mwaka huu ambayo ni ya 38.