• Nairobi
  • Last Updated April 23rd, 2024 9:40 PM
AKILIMALI: Kilimo cha karakara kina mapato ya haraka

AKILIMALI: Kilimo cha karakara kina mapato ya haraka

Na SAMMY WAWERU

WALIOFANIKISHA kilimo cha karakara wanatolea maoni kusema ni mojawapo ya mimea rahisi kukuza na yenye mapato ya haraka.

Matunda haya hayana kizungumkuti cha kupata soko kwa sababu ya faida zake lukuki kimapato na kiafya.

“Matunda ya karakara hayana ushindani sokoni, ni mithili ya mahamri moto. Uhaba wa shamba kupanua kilimo chake ndio kizingiti kikuu,” anasema Bw David Karira, mkulima wa Nyeri.

Mbali na kupanda karakara, mwanazaraa huyu amepamba shamba lake kwa matunda yanayoaminika kuongeza damu mwilini, Tomarillo.

Bi Agnes Omingo mkulima mwingine wa matunda haya kaunti ya Kajiado, anasema kilimo chake hakina ugumu wowote ule na isitoshe huchukua nafasi ndogo.

“Huhitaji mamia ama maelfu ya ekari za shamba kuyapanda. Kipande kidogo tu na utajionea mwenyewe,” aeleza Agnes, akidokeza kwamba ameyapanda kwenye nusu ekari.

Wakulima hawa kwa kauli moja wanaafikiana kwamba cha muhimu katika ukuzaji wa karakara ni matunzo yake. Kulingana na wataalamu wa kilimo, ufanisi wa matunda haya unanogeshwa na maji na mbolea.

“Kinachohitajika sana ni kuyatunza kwa maji ya kutosha na kuyalisha mlo; mbolea, hasa ile hai wakati wa upanzi,” asema mtaalamu Daniel Mwenda, hasa ukuzaji wa matunda. Kabla ya kuzamia katika kilimo hiki, mkulima anashauriwa kujua kiwango cha asidi cha mchanga (pH) anaonuwia kuyapanda.

Bw Mwenda anaeleza kwamba mchanga pia unapaswa kutunzwa kwa kutumia mbolea hai na iliyoiva sawa. Aidha, anahimiza mkulima kuhakikisha kiwango cha madini ya Potassium na Calcium katika mchanga kinaafikiwa ipasavyo.

Upanzi

Shamba linapolimwa, mashimo yenye urefu wa futi tatu kuenda chini, na futi mbili upana ndiyo yanapendekezwa kuandaliwa.

“Mashimo yawe na umbali wa mita tano kutoka moja hadi lingine. Mstari wa laini ya mashimo hadi mwingine uwe na nafasi ya mita tatu,” anashauri mtaalamu Mwenda.

Kulingana na maelezo ya mdau huyu ni kwamba mchanga uliochimbwa shimoni uchanganywe vyema na mbolea, kisha mchanganyiko huo urejeshwe kufikia kimo cha mita mbili. Unapendekezwa kumwagilia mashimo maji kabla ya upanzi.

“Mita moja iliyosalia ni ya kutunza mikarakara kwa maji na mbolea,” asema Mwenda.

Kwa kura karakara hutambaa, husimamishwa kwa vikingi vyenye urefu wa karibu mita 2.5. Funga nyaya za kuyatambisha kutoka kikingi kimoja hadi kingine, mkulima akishauriwa kuyasaidia kutambaa kila mikarakara inapoendelea kukua. Hatua hii huiwezesha kuongeza kiwango cha mazao.

Huanza kuchana maua baada ya miezi saba hivi ya upanzi. Steji hii ni dalili ya kuanza kuzalisha matunda. Ekari moja ina uwezo wa kusitiri karibu mikarakara 600. Mti mmoja unakadiriwa kuzalisha zaidi ya kilo 20 kwa msimu.

Kilo moja ya karakara nchini inagharimu karibu Sh120, ingawa Bw Mwenda anasema bei hii inategemea msimu na maeneo. Maeneo ya Nyeri, Kericho, Embu, Meru, ndiyo yanafahamika kwa kilimo cha matunda haya.

Mdau huyu anashauri wakulima kukumbatia uzalishaji wa karakara za kupandikiza (grafting). Karakara za rangi ya zambarau, zenye asili ya Kenya na manjano ndizo hupandikizwa. Za manjano zina asili ya Tanzania.

You can share this post!

GSU yapata ushindi wa kwanza voliboli ya Afrika

MUTANU: Tukabiliane na mabadiliko ya anga kuzuia magonjwa

adminleo