• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 6:21 PM
MUTANU: Tukabiliane na mabadiliko ya anga kuzuia magonjwa

MUTANU: Tukabiliane na mabadiliko ya anga kuzuia magonjwa

Na BERNARDINE MUTANU

Wananchi sehemu mbalimbali wanazidi kungoja mvua huku matumaini yakizidi kuyeyuka kwa mamilioni wanaokabiliwa na njaa.

Huku mabadiliko ya hali ya hewa yakitarajiwa kuendelea kutatiza wananchi sio Kenya pekee lakini kote ulimwenguni, wananchi wanafaa kujitayarisha vilivyo kukabiliana na hali hiyo kwani zaidi ya njaa, mabadiliko hayo yanatarajiwa kuzua magonjwa tofauti na hali zingine za kiafya.

Kipindupindu ni kati ya magonjwa hayo. Siku kadhaa zilizopita, Serikali ya Kaunti ya Nairobi ilitangaza kuzuka kwa mkurupuko wa kolera jijini.

Wengi wanafahamu kinachosababisha magonjwa kama kipindupindu ni maji chafu, lakini mabadiliko ya hali ya hewa huweza kuchochea ugonjwa kama huo.

Hii ni kutokana na kuwa kiangazi kikubwa kama kinachoendelea kushuhudiwa nchini, ambacho kinahusiana na mabadiliko ya hali ya hewa, husababisha upungufu wa maji safi ya matumizi. Maji yanapopungua, husababisha kuongezeka kwa viini vya magonjwa kama vile bakteria.

Lakini sio tu mabadiliko hayo yanasababisha magonjwa yanayotokana na ukosefu wa maji safi ya kunywa, katika muda wa miezi kadhaa iliyopita, kumekuwa na ongezeko la mbu, ambao husababisha malaria na magonjwa mengine.

Hivi ni kumaanisha kuwa huenda kukawa na visa vingi zaidi vya malaria na magonjwa kama vile dengue na chikungunya, ambayo huambukizwa na mbu.

Katika baadhi ya maeneo, ukosefu wa chakula umefanya watu kudhoofika na hata baadhi ya wengine wamepoteza maisha. Watoto kwa upande wao, wanakabiliwa na utapia mlo huku ukosefu wa chakula ukitarajiwa kuathiri wanawake wajawazito; baadhi yao huenda wakaavya mimba kutokana na hali hiyo.

Zaidi, mabadiliko hayo yamesababisha joto kuongezeka, hali inayoathiri sio tu ufanyakazi, lakini afya ya wananchi. Kulingana na utafiti, joto jingi husababisha kiharusi, ambacho kina uwezo wa kusababisha kifo.

Kwa upande mwingine, mvua inaweza kunyesha kubwa sana na kusababisha mafuriko au gharika, na kusababisha hasara kubwa kama ilivyoshuhudiwa mwaka uliopita.

Hivyo, ni vyema kwa serikali na mashirika husika kujiandaa vilivyo kukabiliana na athari za mabadiliko ya hali ya hewa.

Isiwe wakati wananchi wanapoanza kupoteza maisha ndio serikali inachukua hatua za dharura, ambazo zinapunguza tu athari bila kuwafaidi wananchi kwa muda mrefu.

Kinachohitajika ni hatua madhubuti na za kudumu kukabiliana na athari za mabadiliko hayo. Huku baadhi ya serikali za kaunti zikiwa zimeunda sera kuhusiana na jinsi ya kukabiliana na mabadiliko hayo, kuna baadhi yake ambazo hazina sera zozote kuhusiana na hali hiyo.

Suala hilo limekuwa likizungumziwa kwa muda mrefu lakini huenda halijatiliwa maanani na wahusika wakuu.

Hivi sasa ni wakati wa kulizungumzia zaidi kwani hakuna mtu yeyote ambaye hajashuhudia athari zake. Ni wakati wa kuchukua hatua na kutekeleza makubaliano ya kimataifa kuhusu jinsi ya kupunguza uharibifu wa mazingira, ambacho ndicho kiini kikuu cha mabadiliko ya hali ya anga.

La sivyo, tutazidi kujibizana na kulumbana kuhusu anayestahili kulaumiwa wananchi wanapoanza kupoteza maisha.

You can share this post!

AKILIMALI: Kilimo cha karakara kina mapato ya haraka

WASONGA: Rais akome kuzomea mawaziri hadharani

adminleo