Agizo waliopata D+ wasomee ualimu lafutwa
Na MAUREEN KAKAH
AGIZO lililotaka Taasisi za Mafunzo ya Walimu kushukisha alama zinazohitajika kwa wanafunzi kujiunga nazo, limefutiliwa mbali.
Kwenye makubaliano yaliyotiwa sahihi mbele ya Jaji Mkuu Weldon Korir kati ya Tume ya Kuajiri Walimu (TSC), Waziri wa Elimu, Mamlaka ya Kitaifa ya Viwango vya Elimu na Mwanasheria Mkuu, iliamuliwa agizo hilo litupwe nje.
Ingawa lilikuwa limelenga kuwezesha watu wanaoishi katika maeneo yaliyotengwa kusomea ualimu, suala hilo liliibua mzozo mkali kuhusu uwezo wa walimu watakaoruhusiwa kusomea kozi hizo wakiwa na alama za chini.
Kufuatia hatua hii mpya, alama zitabaki jinsi zilivyokuwa awali kwa yeyote anayetaka kusomea mafunzo ya ualimu ambayo huwa ni alama ya C katika Mtihani wa Kitaifa wa Shule za Upili (KCSE).
“Ilani ya kisheria nambari 118 ya 2018 iliyodai kuipa TSC na Waziri wa Elimu mamlaka ya kutathmini viwango vya elimu na mafunzo ya watu wanaoajiriwa kuwa walimu sasa imefutiliwa mbali,” akasema Jaji Korir.
Siku chache kabla aliyekuwa Waziri wa Elimu, Bi Amina Mohamed kuondoka katika wizara hiyo, alitoa agizo hilo ambalo lilipelekea TSC kuwasilisha malalamishi kadhaa mahakamani.
TSC ilikuwa pia imelalamika kwamba hitaji la wanaotaka kusomea ualimu itakuwa D+ badala ya C kwa wanaotaka cheti cha P1 na wanaotaka diploma kuhitajika kupata alama ya C- badala ya C+ katika kaunti 17 zilizotengwa.
Kesi nyingine iliwasilishwa na wabunge kutoka kwa maeneo ya jamii za wafugaji ambao waliunga mkono uamuzi wa kuteremsha alama zinazohitajika kwa wanaotaka kujiunga na taasisi za mafunzo ya walimu.