Habari Mseto

Mwanaharakati ataka Wangamati ang'olewe mamlakani

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na DENNIS LUBANGA

GAVANA wa Bungoma, Bw Wycliffe Wangamati yuko hatarini kung’olewa mamlakani kwa madai ya utumizi mbaya wa mamlaka.

Hii ni baada ya mwanaharakati wa kutetea haki za binadamu katika eneo hilo, Bw Moses Wanjala Lukoye, kuwasilisha ombi katika Bunge la Kaunti ya Bungoma kutaka gavana huyo aondolewe.

Kulingana na Bw Lukoye anayetoka Wadi ya Maraka iliyo eneobunge la Webuye, gavana huyo anayehudumu kipindi chake cha kwanza alikiuka Sehemu ya 107 (c) ya Sheria ya Usimamizi wa Fedha za Umma ya 2012 inayohitaji mishahara na marupurupu ya watumishi wa umma isiwe zaidi ya asilimia 35 ya mapato ya kaunti.

Kwenye kikao cha wanahabari Jumanne baada ya kuwasilisha ombi lake kwa Afisi ya Karani wa Bunge, Bw Lukoye alisema Bw Wangamati alitumia vibaya mamlaka yake kwa kuajiri watu wasio na ujuzi wa kitaaluma na kufanya mapendeleo kujinufaisha kibinafsi.

“Alikiuka sheria kwa kuajiri watu ambao walikuwa wameshikilia nyadhifa kwenye Chama cha Ford Kenya,” akadai Bw Lukoye.

Alimkosoa gavana pia kwa kubuni nyadhifa ambazo kulingana naye si halali, kama vile Afisa Mkuu katika Afisi ya Naibu Gavana, Afisa Mkuu katika Afisi ya Katibu wa Kaunti, Naibu Katibu wa Kaunti, Kasisi wa Kaunti, Katibu wa Uwekezaji, na Naibu Mkuu wa Wafanyakazi ambaye pia ni katibu wa kibinafsi wa gavana.

Kwenye ombi lake, Bw Lukoye pia alimkosoa Bw Wangamati kwa kubuni kitengo cha utoaji huduma ambacho alisema kinatekeleza kazi sawa na zile za bodi ya huduma za umma katika kaunti na idara ya kaunti inayosimamia masuala ya umma.