• Nairobi
  • Last Updated April 19th, 2024 3:53 PM
Ahadi za Rais bungeni bado hewa

Ahadi za Rais bungeni bado hewa

Na LEONARD ONYANGO

TANGU alipochukua hatamu za uongozi mnamo 2013, Rais Uhuru Kenyatta amekuwa akiahidi Wakenya mengi kupitia hotuba zake za kila mwaka Bungeni.

Alhamisi, Rais Kenyatta atahutubia Bunge kwenye hafla ambayo hutumia kuelezea mipango yake inayolenga kuboresha uchumi, usalama, maslahi ya jamii na kukabiliana na ufisadi.Licha ya kuwa amepiga hatua katika kutekeleza baadhi ya ahadi, bado kuna nyingi ambazo zimebaki hewa.

2014: Rais aliahidi kuweka kamera za CCTV katika miji yote mikuu kote nchini ili kukabiliana na uhalifu.

Lakini takwimu za polisi kuhusu uhalifu zinaonyesha kuwa visa vya uhalifu vinaongezeka kila mwaka katika miji.

Kwa mfano, takwimu za polisi kuhusu hali ya usalama zinaonyesha kuwa visa vya uhalifu viliongezeka kutoka 77,992 mnamo 2015 hadi 76,986 mwaka wa 2017.

Rais Kenyatta pia aliahidi kuwa mawaziri wake wangepunguziwa mshahara kwa asilimia 10 huku yeye pamoja na naibu wake William Ruto wakipunguziwa kwa asilimia 20.

Ahadi hiyo haikutimizwa na badala yake ripoti ya Mkaguzi wa Hesabu za Serikali, Edward Ouko iliyotolewa Juni 2016, ilionyesha yeye na naibu wake walilipwa mishahara na marupurupu mara nne ya kiwango kilichowekwa na Tume ya Kutathmini Mishahara ya Watumishi wa Umma (SRC).

Kulingana na ripoti hiyo, Rais Kenyatta na Dkt Ruto walifaa kulipwa jumla ya Sh36 milioni mnamo 2016, lakini badala yake walilipwa Sh148 milioni.

2015: Rais Kenyatta aliomba Wakenya msamaha kwa dhuluma za kihistoria zilizotekelezwa na serikali zilizotangulia.

Alisema kuwa angetenga Sh10 bilioni ambazo zingetumika kuwalipa fidia waathiriwa wa dhuluma za kihistoria. Wakati huo huo, aliwasihi wabunge kuhakikisha kuwa ripoti ya Tume ya Ukweli, Haki na Maridhiano (TJRC), imetelekezwa.

Miaka mitano baadaye, ripoti ya TJRC ingali haijatekelezwa.

2016: Rais Kenyatta aliahidi kuwa kila mwanafunzi wa Darasa la Kwanza angepewa kipakatalishi. Hata hivyo, si wanafunzi wote waliopokea vifaa hivyo na sasa mpango huo umeacha kutekelezwa.

2017: Rais aliahidi kuwakamata walanguzi wa dawa za kulevya Pwani.

“Ninahakikishia familia za vijana ambao maisha yao yameharibika kutokana na matumizi ya mihadarati kuwa tutawakamata walanguzi. Watalipia uovu ambao wametendea watoto wetu,” akasema Rais Kenyatta.

Kufikia sasa wakazi wa Pwani wangali wanangojea serikali kutimiza ahadi hiyo. Takwimu za Mamlaka ya Kudhibiti Matumizi ya Dawa za Kulevya (Nacada) zinaonyesha idadi ya vijana wanaotumia mihadarati imeongezeka.

2018: Rais alisema Wakenya wangependa kuona gharama ya maisha ikipungua: “Hatuwezi kuendelea kuwa na taifa lenye wakulima maskini wasioweza kulipa hata gharama ya matibabu au kulisha familia zao.”

Licha ya hakikisho hilo, wakulima wanaendelea kuhangaika. Gharama ya maisha nayo imepanda.

You can share this post!

UHALIFU KISAUNI: Wanafunzi wa TUM wamlilia Mutyambai...

Shujaa matumaini tele watawika raga ya Hong Kong 7s

adminleo