Kimataifa

Bouteflika asalimu amri, spika atarajiwa kutwaa hatamu

April 3rd, 2019 Kusoma ni dakika: 2

NA MASHIRIKA

SPIKA wa Seneti ataongoza Algeria kwa muda huku nchi hiyo ikiandaa mikakati ya kuchagua kiongozi mpya baada ya kujiuzulu kwa Rais Abdelaziz Bouteflika, mnamo Jumanne.

Kulingana na Katiba ya Algeria, spika wa Seneti Abdelkader Bensalah ndiye anastahili kuapishwa kuwa kaimu rais kwa siku 90 kabla ya kiongozi mpya kuchaguliwa.

Bensalah, 77, amekuwa spika wa bunge la juu kwa kipindi cha miaka 17 na ndiye amekuwa akimwakilisha Bouteflika katika hafla mbalimbali nchini humo na ughaibuni tangu kiongozi huyo kuugua maradhi ya kiharusi mnamo 2013.

Bensalah amewahi kuwa mbunge, balozi na seneta.

Shangwe, nderemo, vigelegele na nyimbo za ushindi zilihanikiza katika mji wa Algiers, Jumanne, mara tu baada ya Rais Abdelaziz Bouteflika kutangaza kujiuzulu.

Rais Bouteflika, 82, alitangaza kujiuzulu kupitia barua iliyochapishwa na shirika la habari la serikali, APS.

Alijiuzulu takribani siku mbili baada ya mkuu wa majeshi kutaka aondolewe kwa nguvu mamlakani.

Kiongozi huyo alijiuzulu mapema kabla ya kukamilisha muhula wake Aprili 28, mwaka huu.

“Lengo langu ni kurejesha utulivu miongoni mwa wananchi ili kwa pamoja tuweze kupeleka Algeria mbele kimaendeleo,” akasema Bouteflika katika barua yake ya kujiuzulu kwa kiongozi wa Baraza la Kikatiba.

“Nimechukua uamuzi huu ili kuzuia nchi yetu kujitosa katika vurugu ambazo huenda zikasababisha uharibifu wa maisha na mali ya watu,” akaongezea.

Tangu kutangaza kung’atuka Jumanne, raia wa nchi hiyo bado wangali wanasherehekea huku wakipeperusha bendera za nchi hiyo katika mji wa Algiers.

Kujiuzulu kwa Bouteflika ambaye amekuwa akiongoza nchi hiyo akiwa kitandani tangu 2013, kunamaanisha kwamba uongozi wake umefikia kikomo.

Bouteflika aliingia mamlakani mnamo 1999 na baadhi ya wanadani wake wa kisiasa walianza kumtoroka kutokana na maandamano yaliyoanza Februari, mwaka huu. Waandamanaji walimtaka kung’atuka mamlakani huku wakisema ameshindwa kuongoza baada ya kuwa mgonjwa kwa miaka mingi.

Mkuu wa Majeshi Jenerali Ahmed Gaid Salah ni miongoni mwa wandani wa Bouteflika waliomtoroka na kuanza kumpinga.

Salah, wiki iliyopita alitaka Bouteflika atimuliwe kwa nguvu kutoka mamlakani kutokana na kigezo kwamba ameshindwa kuongoza.

Mshauri mkuu wa kiongozi huyo mkongwe alikuwa ndugu yake mdogo Said Bouteflika, 61, ambaye hapo awali alikuwa akipigiwa upatu kumrithi.

Gaid Salah aliteuliwa kuongoza jeshi mnamo 2004 na amekuwa mwandani wa Bouteflika kwa miaka mingi.