• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
Harambee Stars yateremka nafasi mbili viwango vya ubora Fifa

Harambee Stars yateremka nafasi mbili viwango vya ubora Fifa

Na GEOFFREY ANENE

TIMU ya taifa ya Kenya, Harambee Stars imeteremka nafasi mbili kwenye viwango vya ubora wa Shirikisho la Soka Duniani (FIFA) vilivyotangazwa Aprili 4, 2019.

Vijana wa kocha Sebastien Migne wako katika nafasi ya 108 duniani kutoka 106. Kenya ilikuwa na alama 1210 viwango hivi vilipotangazwa mara ya mwisho mnamo Februari 7, lakini sasa zimepungua hadi 1202.

Kuteremka kwa Kenya katika viwango hivi vya mataifa 206 kumechangiwa na Stars kupoteza mechi yake ya mwisho ya Kundi F ya kufuzu kushiriki Kombe la Afrika (AFCON) pale ilipolemewa 1-0 na Ghana mjini Accra mnamo Machi 23.

Senegal imesalia ya kwanza barani Afrika na katika nafasi ya 23 duniani baada ya kupaa nafasi moja. Tunisia haijasonga kutoka nafasi ya pili Afrika katika nafasi ya 28 duniani.

Nigeria imepiga hatua nne mbele na kutulia katika nafasi ya tatu Afrika na 42 duniani.

Inafuatiwa na Morocco ambayo imeteremka nafasi mbili hadi 45 duniani, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo iko juu nafasi tano hadi nambari 46 duniani nayo Ghana ilinufaika na masaibu ya Kenya kuimarika kutoka 52 hadi 49 duniani.

Cameroon pia imeimarika katika viwango hivi ikiruka juu nafasi mbili hadi nambari 54 duniani. Inafuatiwa na wenyeji wa AFCON 2019, Misri, ambao wamekwamilia nafasi ya 57 duniani.

Burkina Faso na Mali zinafuata katika nafasi ya tisa na 10 mtawalia. Burkina Faso imepaa nafasi nne nayo Mali imesalia ya 10. Mabingwa wa Afrika mwaka 2017, Ivory Coast wanashikilia nafasi ya 11 baada ya kuruka juu nafasi moja.

Uganda bado inaongoza eneo la Afrika Mashariki na Kati (Cecafa). Hata hivyo, imeteremka nafasi mbili kwenye jedwali la dunia hadi nambari 79.

Ilipoteza 3-0 dhidi ya Tanzania katika mechi yake ya mwisho ya kufuzu kushiriki AFCON na kuwezesha Tanzania kuingia kipute hiki kwa mara yake ya pili katika historia yake na ya kwanza tangu mwaka 1980.

Kenya inasalia ya pili Cecafa baada ya kushuka nafasi mbili hadi 108 duniani. Inafuatiwa na Sudan (130 duniani baada ya kuteremka nafasi tatu), Tanzania (nafasi sita juu hadi 131 duniani), Burundi (136 duniani kutoka 138) nayo Rwanda imeshuka nafasi tatu hadi nambari 138 duniani.

Hali afadhali kwa Ethiopia

Ethiopia iko juu nafasi moja hadi 150 duniani, Sudan Kusini ni ya 167 duniani baada ya kushuka nafasi tatu, Djibouti imesalia ya 197 duniani nazo Eritrea na Somalia zinavuta mkia katika nafasi ya 203.

Hakuna mabadiliko katika nafasi tatu za kwanza duniani ambapo Ubelgiji, Ufaransa na Brazil zinafuatana katika usanjari huo.

Uingereza imerukia nafasi ya nne na kusukuma Croatia hadi nafasi ya tano sawa na Uruguay ambayo imeruka Ureno na kutulia nafasi ya sita na kusukuma Wareno hadi nafasi ya saba.

Uswizi, Uhispania, Denmark na Argentina zimekwamilia nafasi nne zinazofuata.

Viwango hivi vipya vinatarajiwa kutumiwa na Shirikisho la Soka barani Afrika (CAF) itakapokuwa ikifanya droo ya dimba la AFCON hapo Aprili 12 jijini Cairo.

Eneo la Cecafa lina mataifa manne katika kipute hicho. Mataifa hayo ni Uganda, Kenya, Tanzania, na Burundi.

You can share this post!

AKILIMALI: Anaona akifika mbali kwenye ukuzaji karakara

SHANGAZI AKUJIBU: Mke ananidharau kwani ana pesa nyingi...

adminleo