Bouteflika hatimaye aomba raia wake msamaha
NA MASHIRIKA
RAIS anayeondoka wa Algeria Abdelaziz Bouteflika amewaomba msamaha raia wa nchi kwa kutowajibikia majukumu yake vilivyo kupitia barua iliyochapisha jana kwenye gazeti la serikali.
Bouteflika,82 hata hivyo aliwashukuru wananchi kwa kuunga mkono utawala wake wa miaka 20 japo akakiri kwamba alikumbana na masaibu tele wakati uongozi wake ulikuwa ukielekea ukingoni.
“Kosa ni kwa kila mwanadamu, nawaomba msamaha kwa kufeli haswa siku za mwisho mwisho kabla kujiuzulu kwangu. Najivunia ufanisi tuliopiga katika kipindi cha miaka 20 kama Rais wenu na naondoka mamlakani bila hofu wala uoga wowote,”
“Nashukuru sana kwa uungwaji mkono wenu. Ni matumaini yangu kwamba nchi hii itasalia ikiwa imeungana wala msikubali tofauti mbalimbali kuwagawanya,” ikasema barua hiyo.
Rais huyo alitangaza kujiuzulu wadhifa wake siku ya Jumatano baada ya wananchi wa Algeria kushiriki maandamano makubwa ya wiki sita kupinga utawala wake.
Kujiuzuli kwa Rais Bouteflika kulijiri wiki moja baada ya Mkuu wa Majeshi Jenerali Ahmed Gaed Salah kumtaka abanduke uongozini kutokana na kuchacha kwa maandamano ilipobainika alikuwa na nia fiche ya kusalia madarakani.