62 waangamia kutokana na vita vya kijamii, ugaidi
NA AFP
WIZARA ya Usalama wa Ndani nchini Burkina Faso imetangaza kwamba, watu 62 wamefariki wiki hii kutokana na ghasia za kijamii na uvamizi wa makundi ya kigaidi Kaskazini mwa nchi hiyo.
Kulingana Waziri wa Usalama wa Ndani Simeon Sawadogo, ghasia zilizozuka Jumapili na Jumanne katika mji wa mpaka wa Arbina ndizo zilichangia maafa hayo.
“Vifo 32 vimeripotiwa kutokana na uvamizi wa magaidi na vingine 30 vimetokana na vita vikali kati ya jamii za Kouroumba, Peuls na Mosii. Vile vile, watu wengine tisa walitekwa nyara na magaidi baada ya wavamizi waliojihami kwa silaha hatari kuwakimbiza watu kutoka makwao na kuwaua wengine,” Bw Sawadogo akasema kupitia hotuba iliyopeperushwa moja kwa moja na runinga zote za Burkina Faso.
Majangili waliojihami vikali Jumapili walivamia kijiji cha Hamkan, kilichoko umbali wa kilomita nne pekee kutoka mji wa Arbinda kisha kumuua Kiongozi wa Dini ya Kiislamu Sheikh Werem, mwanawe pamoja na mpwa wake.
Mauaji ya Shekhe huyo yalizua mapigano makali kati ya jamii hizo hasimu kila moja ikitaka kulipiza kisasi kwa kuuawa kwa watu wao. Wanakijiji walilazimika kutorokea usalama wao hadi mji wa Arbinda vita vilipochacha.
“Baada ya kuuawa kwa Shekhe Werem, mapigano makali yalizuka kati ya jamii tatu zinazoishi karibu na mji wa Arbinda, kila jamii ikipania kulipiza kisasi ikilaumu nyingine kwa vifo hivyo na vingine vilivyotokea siku za nyuma. Kwa sasa, hali ni mbaya na suala hili linafaa kushughulikiwa kwa dharura kwa sababu hakuna raia ambaye amehakikishiwa usalama wake,” akaongeza Bw Sawadogo huku akisisitiza serikali inafanya juu chini kurejesha hali ya utulivu na kuwasaidia waliotoroka kujikimu kimaisha.
Burkina Faso imekuwa ikikumbana na uvamizi wa mara kwa mara kutoka kwa makundi ya kigaidi ya Kiislamu ya Ansaroul na GSIM kwa muda wa miaka minne iliyopita.
Hata hivyo, Bw Sawadogo alisisitiza kuwa lengo kuu la magaidi hao ni kuzua uhasama kati ya jamii mbalimbali kisha kutwaa usimamizi wa kuongoza mji wa Arbinda.
“Lengo kuu la magaidi ni kuzua ugomvi kati ya jamii hizo tatu kisha kuzitawal,” akasisitiza Bw Sawadogo.