Habari Mseto

Agizo la Rais laletea kiwanda cha nguo Kitui sifa kubwa

April 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na KITAVI MUTUA

AGIZO la Rais Uhuru Kenyatta kwamba sare zote za maafisa wa utawala wa serikali ziwe zikitengenezwa katika Kaunti ya Kitui limeonekana kukipatia sifa kubwa kiwanda kipya cha nguo katika kaunti hiyo inayosimamiwa na Gavana Charity Ngilu.

Rais Kenyatta alisema mavazi ya maafisa wa utawala wakiwemo maelfu ya machifu na manaibu wao yatakuwa yakitengenezewa katika kiwanda cha nguo cha Kitui County (KICOTEC).

Hatua hii imenuiwa kupiga jeki mpango wake wa kukuza viwanda humu nchini chini ya ajenda kuu ya utengenezaji bidhaa.

Alitoa agizo hilo Jumanne wakati alipoongoza uzinduzi wa mfumo mpya wa kusajili watu wa NIIMS katika soko la Masii, Kaunti ya Machakos.

Kitengo cha utawala wa serikali ni kimojawapo kilicho chini ya Wizara ya Usalama wa Ndani na Usimamizi wa Serikali Kuu ambapo kuna maafisa 12,575.

Wanajumuisha wasimamizi wanane wa maeneo ya nchi yaliyokuwa mikoa zamani, makamishna 47 wa kaunti, manaibu makamishna 289 wa kaunti, wasaidizi 831 wa makamishna wa kaunti, machifu 3,256 na manaibu chifu 8,145.

Agizo hilo la Rais Kenyatta linatarajiwa kusaidia Kaunti ya Kitui kujiongezea mapato.

Kama kila chifu na manaibu wake watatengenezewa sare mbili mbili kwa karibu Sh10,000 kila moja, Kaunti ya Kitui itatarajia kupata Sh228 milioni mwaka huu pekee.

Bi Ngilu alisema serikali yake inajadiliana na afisi ya Waziri wa Usalama wa Ndani, Dkt Fred Matiang’i kuhusu jinsi mpango huo utakavyotekelezwa.