HabariSiasa

Katu sitaacha kutangatanga, asema Ruto

April 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na NDUNGU GACHANE

NAIBU Rais William Ruto ameapa kuendelea kuzuru sehemu mbalimbali nchini licha ya pingamizi kutoka kwa baadhi ya viongozi wa Jubilee na upinzani.

Akizungumza katika Kaunti ya Murang’a Jumatano, Dkt Ruto alisema lengo lake ni kusambaza maendeleo kila pembe ya nchi, na hatakubali yeyote kumzima.

Alikashifu vikali viongozi wa kundi la ‘Kieleweke’ na upinzani akidai wamepanga njama za kuzima azma yake ya kuwania urais 2022, akisema kuwa hawatafaulu.

‘Kieleweke’ ni kundi katika eneo la Mlima Kenya ambalo limejitokeza kumpinga Dkt Ruto na linaongozwa na Mbunge wa kuteuliwa Maina Kamanda, Ngunjiri Wambugu (Nyeri Mjini), Muturi Kigano (Kangema) kati ya wengine.

Akihutubu katika hafla ya kuchangisha pesa katika Shule ya Upili ya Wasichana ya Kamahuha, Dkt Ruto alisema viongozi hao wamepotoka na hawatafaulu katika juhudi zao.

“Kuna watu ambao wameungana na upinzani na kubuni vuguvugu la kupinga Ruto. Wanapaswa kungoja muda ufaao wa kufanya siasa. Wanapaswa kufahamu Wakenya watawapigia kura kwa msingi wa utendakazi wao lakini sio kwa kujiunga na kundi ambalo lengo lake kuu ni kusambaratisha chama chetu,” akasema.

Dkt Ruto alisema wanasiasa hao wanapaswa kukoma kuzungumzia siasa za 2022, kwani wananchi ndio wataamua kuhusu kiongozi watakayemchagua.

Aliwaonya viongozi wa Jubilee dhidi ya kujihusisha na upinzani akisema ajenda yao ni kuharibu Chama cha Jubilee na kuzua migawanyiko serikalini.

Kando na hayo, alishikilia kwamba ujenzi wa mabwawa ya Arror na Kimwarer utaendelea, licha ya pingamizi za baadhi ya watu.

Pia alipuzilia mbali mwafaka wa kisiasa kati Rais Uhuru Kenyatta na kiongozi wa ODM, Raila Odinga, akisema kuwa Bw Odinga alishindwa kutekeleza majukumu yake ambapo sasa anajifanya kutoa ushauri kwa serikali ya Jubilee.

Wabunge walioandamana naye pia walilishambulia vikali kundi hilo la Kieleweke.

“Ni jambo la kuchekesha kuona kundi hilo likizuru makanisa kumshambulia Dkt Ruto badala ya kupeleka ajenda za maendeleo,” akasema Mbunge wa Maragua, Mary Waruinge.

Wengine walioandamana naye ni wabunge Rigathi Gachagua (Mathira), Sabina Chege (Murang’a), Jonah Mburu (Lari), Joyce Korir (Bomet), Faith Gitau (Nyandarua) kati ya wengine.