Habari MsetoSiasa

Upinzani waunga Rais mkono katika vita dhidi ya ufisadi

April 4th, 2019 Kusoma ni dakika: 1

Na PETER MBURU

VIONGOZI mbalimbali Alhamisi waliunga mkono Rais Uhuru Kenyatta kwa kujitolea kwa serikali yake katika kupigana na ufisadi.

Viongozi wa upinzani Raila Odinga, Kalonzo Musyoka, Musalia Mudavadi na Moses Wetangula, ambao walikuwa bungeni, walisema Rais alikuwa sawa, huku wakivamia viongozi ambao wamekuwa wakikosoa vita dhidi ya uhalifu huo.

Bw Odinga alisema hakufai kuwa na uingiliaji katika vita dhidi ya ufisadi, na akataka asasi za kuchunguza kesi za ufisadi kuziharakisha kwani Wakenya wanakufa moyo.

“Rais amesema hakutakuwa na hali ya kutatiza vita dhidi ya ufisadi, na ninamuunga mkono kabisa. Wakenya wanakasirishwa na muda mrefu unaotumika kufanya uchunguzi, na hivyo kasi ya kufanya uchunguzi na kushtaki kesi hizi inafaa kuongezwa,” akasema Bw Odinga.

“Tunafaa kusonga kwa kasi kuhakikisha kuwa watu wanaoendelea kuiba mali ya nchi hii na kunyima nchi maendeleo wanakumbana na sheria haraka iwezekanavyo,” akasema.

Bw Musyoka naye aliwakashifu viongozi ambao wamekuwa wakishambulia asasi za kuchunguza visa vya ufisadi, akisema Wakenya wanawamulika.

“Sikutarajia Rais awafute watu kazi, lakini nadhani kwa kusema asasi zinazohusika na vita hivi ziimarishwe na zipewe heshima, ameweka wazi kujitolea kwake. Natarajia kuanzia kesho kuendelea mbele watu watakamatwa, wapelekwe mahakama na kufungwa jela,” akasema Bw Musyoka.

Bw Wetangula alikubaliana na Rais kuwa vita dhidi ya ufisadi vinafaa kuendeshwa kisheria, akisema taifa lilikuwa linaelekea kupoteza mwelekeo, na akataka asasi za uchunguzi kufanya kazi ipasavyo, ili kesi zinazofikisha kortini zizae matunda.

“Asasi za kuchunguza ufisadi zifanye kazi kwa busara na kikamilifu, ili zipeleke kortini kesi zenye uzito ambao utafanya watu kufungwa,” akasema Bw Wetangula.