Wanahabari wa kike wahimizwa kutia bidii, inalipa
Wakihutubu Alhamisi katika mkutano wa kujadili nafasi wanahabari wa kike kupata vyeo vya juu katika mashirika ya habari nchini wataalamu katika sekta uanahabari hata hivyo waliwataka wasimamizi wa vyombo vya habari kutoa mazingira faafu kwa wanahabari wa kike kuweza kunawiri sawa na wenzao wa kiume.
Mkutano huo ulifanyika katika Hoteli ya Serena, Nairobi kwa udhamini wa Chuo Kikuu cha Aga Khan.
“Nilipanda ngazi katika taaluma ya uanahabari hadi kufikia katika kiwango hiki kutokana na bidii na kujitolea kwangu katika majukumu yangu, sio kwa sababu mimi ni mwanamke. Wenzetu ambao ni limbukeni katika taaluma hii wanafaa kuiga mfano huu,” akasema Bi Pamela Sittoni ambaye ni Mhariri Mkuu wa Gazeti la Daily Nation.
Bi Sittoni alisema kwa kuzingatia moyo huo atafanya kila awezalo kuwapandisha vyeo wanawake ambao watadhirisha bidii na utendakazi mzuri wanapandishwa vyeo ili waweze kuwa kielelezo nzuri kwa wenzao.
Naye Bw Joe Odindo, amewahi kuwa mhariri msimamizi wa magazeti ya Daily Nation na The Standard alisema idadi ndogo ya wanawake wenye vyeo vya juu katika mashirika ya habari humu nchini inatokena na taasubi za kiume miongoni mwa wasimamizi wa mashirika ya habari.
“Sababu nyingine ni unyanyasaji wa kimapenzi ambao umechangia wanahabari wengi wa kike kugura na kuenda kufanya kazi katika sekta nyinginezo kama vile uhusiano mwema na mashirika ya serikali,” akasema Bw Odindo.
“Maovu kama haya yamewanyima wanahabari wa kike nafasi ya kupandishwa vyeo. Mwelekeo huu unapasa kubadilishwa ili kufikia usawa katika nyanja hii sio tu nchini Kenya bali barani Afrika,” akaongeza.
Wengine
Wengine waliohutubia kikao hicho ni mwanahabari Catherine Gicheru, Mhariri wa gazeti la The Nairobian Quenter Mbori na mchangazi wa masuala ya sera katika Shirika la Amnesty International Bi Joanne Kobuthi.
Utafiti uliofanywa na Shirika Tifa Research mwaka 2018 ulibaini ni asilimia 27 pekee ya nyadhifa za juu katika mashirika ya habari Afrika zinazoshikiliwa na wanawake.