• Nairobi
  • Last Updated April 18th, 2024 11:55 AM
JAMVI: Kinaya Raila kuhubiri umoja nchini ngome yake ikisambaratika

JAMVI: Kinaya Raila kuhubiri umoja nchini ngome yake ikisambaratika

Na CECIL ODONGO na PETER MBURU

HUKU Kinara wa Upinzani nchini Raila Odinga akiendelea kuhubiri injili ya umoja nchini, kaunti za Homabay na Migori ambazo ni ngome yake zinaendelea kukumbwa na migawanyiko ya kisiasa kati ya viongozi wa Chama cha ODM

Katika Kaunti ya Siaya, wakazi wa eneobunge la Ugenya walikaidi wito wa Bw Odinga kumchagua Bw Christopher Karan wa ODM katika uchaguzi mdogo wa ubunge ulioandaliwa Ijumaa, badala yake wakimchagua David Ochieng wa chama cha MDG.

Kushindwa kwa Bw Karan kulikuja kama pigo kubwa kwa Bw Odinga na ODM kwani wametumia muda mwingi kumpigia debe na kumchafua Bw Ochieng, lakini mawimbi ya raia yakapaza sauti yake.

Wakazi wa eneobunge la Embakasi Kusini pia walikaidi wito wa Bw Odinga na ODM kumchagua mwaniaji wa ODM Bw Irshad Sumra siku hiyo, licha ya viongozi takriban wote, wakiongozwa na Bw Odinga kukita kambi huko siku chache kabla ya uchaguzi kumpigia debe.

Matokeo ya chaguzi hizo yamekuja kama ujumbe unaojitokeza wazi kuwa licha ya Bw Odinga kujiweka kipaumbele kupigania umoja wa taifa, boma lake lingali na doa.

Bw Odinga amekuwa akivumisha injili ya umoja na uwajibikaji wa viongozi kwa wapigakura baada ya kuamua kushirikiana na Rais Uhuru Kenyatta katika makubaliano ya ‘handshake’ mwaka uliopita

Lakini katika ngome yake Nyanza, ni kaunti ya Kisumu tu ambayo uongozi wake unaonekana kuwa thabiti, chini ya Gavana Anyang’ Nyong’o.Katika Kaunti ya Homa Bay, Gavana Cyprian Awiti hajaonekana hadharani katika shughuli za umma huku usukani wa kaunti ukiendeshwa na Naibu Gavana Hamilton Orata.

Bunge la Kaunti ya hiyo pia limekuwa likikumbwa na vurugu, madiwani wakizozana na Spika Elizabeth Ayoo na hata pande husika kukabiliana kupitia kesi mahakamani.

Utata huo pia umechangiwa na kampeni za mapema zinazoendelea kushuhudiwa huku Kiongozi wa wachache Bungeni John Mbadi, Mbunge wa Homa Bay mjini Peter Kaluma na Mwakilishi wa kike Gladys Wanga wakitangaza azma zao za kuwania ugavana 2022.

Bi Wanga ameanzisha kipute cha mchezo wa soka kwa jina Wanga Cup ili kujivumisha kwa raia huku Bw Mbadi akipigia upato mfumo mpya wa kugawa mamlaka kati ya jamii ya Waluo na Wasuba kujinadi kwa wapiga kura.

Bw Kaluma naye amekuwa akitumia weledi wake katika masuala ya sheria kuwadhihirishia wananchi kuwa yeye ni mchapakazi.

Ingawa hivyo, duru zinazoeleza kwamba aliyekuwa mwaniaji wa kiti cha ugavana na Mbunge wa zamani wa Kasipul Oyugi Magwanga anapanga kurejea chamani ODM, hali ambayo inatazamiwa kuzidisha zaidi joto la kisiasa katika kaunti hiyo yenye wapigakura wengi zaidi eneo la Nyanza.

Bw Odinga alijaribu kuingilia kati kutuliza hali katika bunge la kaunti ya Homabay, wakati ODM kiliwatimua baadhi ya madiwani wanaohusishwa na vurugu lakini hali haijatulia, ila uhasama kati ya madiwani unaendelea kutokota.

Katika kaunti jirani ya Migori, Gavana Okoth Obado na wabunge wa kaunti hiyo hawapikiki wakaiva kwenye chungu kimoja kutokana na uadui unaodaiwa kuchochewa na tofauti zilizozaliwa na siasa za 2017 kati yake na Seneta Ochillo Ayacko na ODM.

Bw Obado pia haelewani kabisa na wabunge wawili wa jamii ya Kuria, Marua Kitayama wa Kuria Mashariki na Mathias Robi wa Kuria Magharibi.

Wikendi iliyopita katika mazishi ya mamake Bw Kitayama, wabunge Peter Masara (Suna Magharibi), Seneta Mteule Dennitah Ghati, Bw Robi na madiwani kadhaa walilaumu Gavana Obado kwa madai anaitesa jamii hiyo kwa kukataa kupandisha hadhi hadi kiwango cha Manispaa miji ya Isbania na Kehencha.

Gavana huyo pia ameshtumiwa kwa kufadhili genge hatari la ‘Sangwenya’ linalodaiwa kuwashambulia wapinzani wake. genge hilo limewahi kutekeleza uvamizi katika bunge la kaunti mara si moja na kuwachapa madiwani wanaopinga sera za Bw Obado.

Katika mahojiano na jarida la Jamvi, Bw Kitayama alimtaka Bw Odinga kujitokeza hadharani iwapo ameshindwa kumdhibiti Bw Obado ambaye alisema uongozi wake ni wa kidikteta uliojaa unyanyasaji na ukandamizaji wa sauti ya wanaomkosoa.

Kundi la Sangwenya limeteka Migori na hata viongozi wa ODM wanaliogopa. Kila mara kundi hilo huvamia bunge la kaunti na kushambulia madiwani wenye msimamo tofauti na Bw Obado.

Mimi nina machungu kwa sababu hapa Migori mambo yote yameharibika na kila jambo linafanyika kwa mapenzi ya Bw Obado.

Namwomba Waziri wa Usalama wa Ndani Fred Matiang’i awaeleze wenyeji wa Migori iwapo ameshindwa kuikabili Sangwenya. Itabidi tuvumilie tu na mungu ashuke atusaidie kwa kuwa hatuna jingine ila kutii Sangwenya hadi 2022,” akasema Bw Kitayama.

Mbunge wa Suna Magharibi Peter Masara akizungumza na Jamvi alisema mgawanyiko unaoshuhudiwa katika kaunti ya Migori unatokana na ‘kichwa ngumu’ ya Gavana Okoth Obado na uhusiano wake wa karibu na Naibu Rais William Ruto.

“Ni ukweli kaunti za Migori na Homabay zipo nyuma lakini ningependelea sana kuzungumza kuhusu Migori ambayo inasimamiwa na Bw Obado. Huyo Gavana haambiliki hasemezeki tangu aingie ndoa ya kisiasa na Naibu Rais William Ruto na kuanza kumpinga Bw Odinga waziwazi.

Amekuwa akifanya mambo kivyake wala hashauriani na mtu yeyote kuhusu maswala ya kaunti yetu,”“Wabunge wote wa Migori wanalalamika kwamba kazi ya Bw Obado ni kulipiza kisasi dhidi ya wananchi ambao hawakumpigia kura kwa kuwanyima miradi ya maendeleo.

Uchaguzi uliofanyika wa Useneta pia ulizua mgawanyiko zaidi na Bw Obado anatumia genge sugu la Sangwenya kuwachapa wanaokosoa serikali yake. Viongozi wameingiwa uoga kumkosoa kwa hofu ya kushambuliwa na Sangwenya,” akasema Bw Masara.

Mbunge huyo vilevile amefutilia mbali uwezekano wowote wa wabunge wa ODM ‘kuinamia’ Bw Obado akisema gavana huyo amedhihirisha wazi kuwa amegura kambi ya ODM na hana heshima yoyote kwa Bw Odinga.

“Juhudi zetu za kuirai polisi kukabiliana na kundi la Sangwenya hazionekani kuzaa matunda kwa sababu kundi hilo aminifu kwa Bw Obado linaendeleza ukatili Migori. Hata hivyo hatutamwabudu jinsi anavyotaka. Yeye ameenda kwa Bw Ruto wala hatii tena maagizo ya kinara wetu kwa kuwa hana nia ya kusimama ugavana baada ya kumaliza muhula wake wa pili mwaka wa 2022,” akaongeza Bw Masara.

Hata hivyo, mchanganuzi wa masuala ya kisiasa Martin Andati anasema Bw Odinga ana nafasi kubwa ya kumaliza uhasama na kampeni za mapema katika kaunti hizo kwa kuandaa mkutano mkubwa na viongozi wote ili kulainisha mambo na kurejesha utulivu.

“Bw Odinga ndiye kigogo wa siasa za Nyanza na ni wazi kwamba hata Bw Obado akikimbilia kwa Naibu Rais, bado hana mchango wowote wa kisiasa kama Bw Odinga hajastaafu,” akasema.

You can share this post!

JAMVI: Je, Uhuru amenasa Mudavadi na Weta?

FATAKI: Ishara za mume asiyekupenda huonekana mapema

adminleo