HabariSiasa

Handisheki yamuumiza 'Baba'

April 8th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

Na WANDERI KAMAU

USHAWISHI wa kisiasa wa Kiongozi wa ODM, Raila Odinga, umefifia tangu handisheki, wadadisi wa siasa wanaeleza.

Wachanganuzi wanasema kuwa kushindwa kwa ODM katika chaguzi ndogo za maeneobunge ya Embakasi Mashariki na Ugenya kulitokana na Bw Odinga kufungwa mikono na handisheki.

Kwenye chaguzi hizo za Ijumaa, David Ochieng alimshinda mgombeaji wa ODM Chris Karan katika eneo la Ugenya huku Ishard Sumra wa ODM akiangushwa na Julius Mawathe katika Embakasi Kusini.

Hata hivyo, kufifia kwa nyota ya kisiasa ya Bw Odinga kumekuwa ni baraka kwa Naibu Rais William Ruto kwani alipoamua kuzituliza, Dkt Ruto naye aliamua kuzipepeta katika kila pembe ya nchi, ambapo wadadisi wanasema ndiye aliyechangia pakubwa kushindwa kwa ODM katika maeneobunge hayo.

Dkt Ruto amevuna kutokana na handisheki licha ya kuipinga vikali akidai inalenga kumfifisha yeye kisiasa.

Mara baada ya matokeo ya chaguzi hizo kutangazwa, Dkt Ruto aliandika kwenye Twitter yake: “Hongera Ochieng na Mawathe kwa ushindi mliopewa na Mungu. Jameni wacheni Mungu aitwe Mungu.Watu wameamua.”

“Alipoingia kwenye muafaka na Rais Uhuru Kenyatta kupitia handisheki, Raila aliingia kwenye barabara telezi inayomhitaji kutojishughulisha sana na siasa, na badala yake matendo yake yaonyeshe yeye ni kiongozi wa kitaifa,” alisema Prof Amukowa Anangwe.

“Handisheki ilikuja na gharama kubwa ya kisiasa kwa Raila. Amejifunga kiasi kwamba hawezi kusimamia kikamilifu masuala ya chama chake,” anaeleza mchanganuzi huyo.

“Baba (Bw Odinga) amewapuuza wapigakura katika ngome yake ya Nyanza, na pia ameacha kujiuza katika maeneo mengine ya nchi. Sijui anafikiri nyota yake ya kisiasa itang’aa vipi akiwa hafanyi lolote,” akashangaa Mbunge wa Pokot Kusini, David Pkosing.

Tangu Machi 9, 2018 alipoingia kwenye handisheki na Rais Uhuru Kenyatta, Bw Odinga amekaa raha mustarehe akishiriki shughuli za kiserikali huku akiacha kujishughulisha na siasa mashinani.

Kulingana na Mbunge wa Suna Mashariki, Junet Mohamed, kukosekana kwa Bw Odinga kwenye kampeni za Embakasi Kusini na Ugenya ndiyo iliyokuwa sababu kuu ya wagombeaji wa ODM kushindwa.

“Chaguzi za Embakasi Kusini na Ugenya zimeonyesha kuwa neno la Raila ndilo muhimu zaidi katika ODM na miongoni mwa wafuasi wetu,” akasema Bw Junet.

Prof Anangwe anaunga mkono kauli ya Bw Junet, akieleza kuwa kushindwa kwa ODM, hasa katika uchaguzi wa Ugenya, kumeonyesha kuwa bila Bw Odinga chama hicho hakina ushawishi hata katika eneo la Nyanza.

Badala ya kushiriki siasa, Bw Odinga amekuwa kama mmoja wa maafisa wakuu wa serikali akihusika katika hafla za kitaifa na kumwakilisha Rais Kenyatta nje ya nchi.

Wadadisi wanasema kuwa kuna wafuasi wengi wa Bw Odinga ambao hadi sasa hawajakumbatia handisheki.

“Baadhi ya wafuasi wa Raila wangali wamekasirika kutokana na hatua yake kukubali kushirikiana na Uhuru. Imani ya wengi kwake imepungua na anaonekana kama mtu anayechukua hatua bila kuwajali wafuasi wake,” akaeleza Prof Anangwe.

Wengine wamekuwa wakimkosoa Bw Odinga kwa kile wanachokiona usalaliti kwa mwananchi wa kawaida.