• Nairobi
  • Last Updated April 20th, 2024 5:23 PM
‘Tangatanga’ sasa wajiita Yellow Movement

‘Tangatanga’ sasa wajiita Yellow Movement

NA RICHARD MAOSI

KUNDI la kisiasa la ‘Tangatanga’ lilikita kambi Jumapili mjini Nakuru kubuni nembo mpya ya chama cha URP, lakini mara hii likijiita Yellow Movement.

Wakiwa wamevalia jezi za manjano zenye maandishi ya Friends of William Samoei Ruto, walishinikiza kusikizwa na umma wakisema walikuwa tu marafiki wa Naibu Rais.

Kulingana na mwakilishi kutoka eneo la Magharibi Peter Masibo, Yellow Movement ulianza mitandaoni, kabla ya kupata ufuasi uliobuni muungano.

Wanachama walipanga kupatana kwa mara ya kwanza mjini Nakuru na kufanya uteuzi wa nyadhifa. Pia waliweka kanuni na misingi ya chama.

MCA wa wadi ya Kabazi, Peter Mbae aliposema kinara wa ODM Raila Odinga anafaa kugura siasa. Picha/ Richard Maosi

Alex Kiprop alichaguliwa kuwa mwenyekiti, na Leila Mohammed akachukua hatamu za kuhudumu kama katibu mkuu.

Yellow Movement waligawa nchi katika maeneo 14, na kutoa mwakilishi atakayesimamia kila mojawapo,ya sehemu hizo.

“Tumeamua kuwa marafiki wa Dkt Ruto kwa sababu tumeona rekodi yake ya maendeleo,” Bw Masibo alisema.

Aidha mshirikishi wa kitaifa Bw Sandei Muyolo alisema muungano wao unapinga siasa za kueneza chuki katika hafla za matanga na harusi.

Washikadau wa Yellow Movement wakifuatilia hotuba ya viongozi wao. Picha/ Richard Maosi

Pia alimhimiza kiongozi mkuu wa upelelezi (DCI) aendelee kufanya uchunguzi, kwa njia ya uwazi akishirikiana na mahakama kuu akisema hizi ni taasisi huru.

“Tunamhimiza aendelee kupigana na ufisadi lakini kwa kufuata sheria.”

Muyolo alisema mahasidi wakome kumhusisha Dkt Ruto na tuhuma za ufisadi. Kwa upande mwingine alipuuzilia mbali madai kuwa Yellow Movement walikuwa wakifanya kampeni za mapema kwa niaba ya Naibu Rais.

Bw Muyolo alisisitiza kuwa kufikia tarehe 30 Juni, 2019 muungano utakuwa umeimarisha juhudi za kuongeza idadi ya wanachama mashinani, hasa wakilenga kaunti zote 47 nchini.

Bw Sandei Muyolo, mshirikishi wa kitaifa akiwahutubia wanachama kwenye hafla iliyofanyika mjini Nakuru. Picha/Richard Maosi

Taifa Leo Dijitali ilipotaka kubaini mfadhili wa shughuli zao kutalii kila mahali, Bw Muyolo alisema walikuwa wakijifadhili.

Miongoni mwa waliohudhuria ni kiongozi mbishi Peter Mbae, mwakilishi kutoka wadi ya Kabazi, eneo la Solai viungani mwa mji wa Nakuru.

Alimshambulia kinara wa ODM Raila Odinga, akisema ushawishi wake kisiasa ulikuwa umedidimia.

Akitoa mfano wa matokeo ya uchaguzi mdogo kutoka Ugenya na Embakasi ambapo ODM ilibwagwa.

 

You can share this post!

URODA KWA FOLENI: Je, ni rahisi kuacha ukahaba?

Mwanamke wa kwanza kuongoza wanafunzi UoN, uchaguzi wa...

adminleo