UFISADI: Wasilisheni ushahidi, Raila aambia wanasiasa wanaolia
NA CECIL ODONGO
KINARA wa upinzani nchini Raila Odinga Jumatatu aliwataka wanaodai kwamba vita dhidi ya ufisadi vinalenga jamii zao wawasilishe ushahidi kwa vyombo vya kisheria.
Bw Odinga alikanusha madai kuwa vita vinavyoendelea dhidi ya ufisadi vinalenga jamii fulani jinsi imekuwa ikidaiwa na baadhi ya wanasiasa akisema wafisadi hawafai kutumia jamii zao kama ngao ya kujikinga kila mara wanapotajwa kuhusika katika wizi wa mali ya umma.
“Vita vinavyoendeshwa dhidi ya ufisadi havilengi jamii au kabila. Wale wamekuwa wakidai vinalenga jamii zao wanafaa kuwasilisha ushahidi kwa asasi faafu za kisheria kuthibitisha madai yao,” akasema Bw Odinga.
Baadhi ya viongozi wa Chama cha Jubilee wamekuwa wakidai kuwa vita dhidi ya ufisadi vinalenga Naibu Rais Dkt William Ruto na washirika wake wa kisiasa huku wakimlaumu Bw Odinga kwa kutumia mwafaka kati yake na Rais Uhuru Kenyatta kumsawiri Dkt Ruto kama kiongozi fisadi asiyefaa kuchaguliwa kuwa rais mwaka wa 2022.
Akizungumza katika ofisi yake ya Capitol Hill jijini Nairobi alipokutana na viongozi kutoka jamii ya Wakalenjin waliomtembelea, Bw Odinga aliahidi kwamba vita hivyo vitaendelea na wahusika kukabiliwa kisheria iwapo watapatikana na hatia.
Ujumbe wa viongozi, wazee na wafanyabiashara uliokutana na Bw Odinga uliongozwa na Waziri wa zamani Musa Sirma na Katibu Mkuu wa chama cha KANU, Nick Salat. Ujumbe huo uliunga mkono vita dhidi ya ufisadi na kuandaliwa kwa kura ya maamuzi.
“Wale ambao wamekuwa wakitumia jina la Bw Odinga kila mara wanapokabiliwa na shida wanafaa kukoma kufanya hivyo. Sisi tunafahamu vita dhidi ya ufisadi havilengi jamii bali wale wanaopora mali ya umma. Tunamshukuru Rais Kenyatta kwa kuagiza Idara ya Uchunguzi wa Uhalifu wa Uhalifu (DCI) kufanya kazi yake kwa uwazi bila kuingiliwa na yeyote,” akasema Bw Salat.
Aidha, viongozi hao walisema wanaunga mkono ushirikiano kati ya Rais Kenyatta na Bw Odinga na mapendekezo yatakayotolewa na kamati iliyoundwa almaarufu Building Bridges Initiative (BBI).
Vile vile walimtaka Bw Odinga kujumuisha changamoto zinazokabili wakazi wa Bonde la Ufa kama ukame, matatizo yanayozonga wakulima wa majani chai, mahindi, ngano na kilimo cha ufugaji katika mapendekezo ya kamati ya BBI.