• Nairobi
  • Last Updated April 24th, 2024 1:05 PM
AUNTY POLLY: Chunusi hazikomi kunitokea usoni…

AUNTY POLLY: Chunusi hazikomi kunitokea usoni…

Na PAULINE ONGAJI

KWA wiki kadha sasa nimekuwa nikikumbwa na chunusi katika uso wangu kiasi cha kunifanya nikose starehe. Naomba ushauri wa kukabiliana na tatizo hili.

Mariam, 17, Mombasa

Vijana wengi wakiwa katika umri huu hutatizika na suala hili kiasi cha kupoteza ujasiri wa kuzungumza na watu. Hata hivyo, ningependa kukuambia kwamba ukiwa katika umri wa kubalehe ni kawaida kukumbwa na chunusi kwani inaashiria kwamba unazidi kukomaa. Kuna mbinu ambazo waweza kutumia kupunguza makali ya chunusi. Kwanza, nawa uso angaa mara mbili kwa siku kwa kutumia sabuni na maji yaliyopashwa moto. Unapochagua sabuni ni jambo la busara kutafuta ushauri wa mtaalam wa masuala ya ngozi. Pili, koma kugusagusa uso wako kwani unapofanya hivi unatatiza ngozi na vinyweleo. Tatu, punguza matumizi ya vipodozi lakini ikiwa lazima uvitumie nunua vya ubora wa hali ya juu, na uhakikishe kwamba unaviondoa kabla ya kulala. Nne, unapotumia mafuta ya nywele hakikisha kwamba hazigusani na uso wako.

Rafiki yangu wa karibu alifariki majuma matatu yaliyopita. Nimeshindwa kuendelea na maisha kwani kila mara najipata nikilia. Baadhi ya jamaa na marafiki wananiambia kwamba huo ni utoto na sharti nirejelee maisha ya kawaida haraka iwezekanavyo. Nifanyeje?

Betty, 17, Nairobi

Pole kwa kifo cha rafiki yako. Japo majuma matatu ni machache sana kumsahau mtu, ningependa kukujulisha kwamba watu huwa na mbinu tofauti za kuomboleza. Kuna baadhi ya watu ambao huwa rahisi kuendelea na maisha baada ya msiba, ilhali kuna baadhi wanaozidi kuhuzunika kwa muda mrefu. Ni kawaida kuomboleza, lakini pia sharti maisha yaendelee. Usiache kumbukumbu ulizo nazo kumhusu rafiki yako zitawale maisha yako kwani kifo ni kitu ambacho hauwezi kubadilisha. Wakati mmoja itakulazimu uendelee na maisha. Ningekuomba upate mawaidha kutoka kwa mshauri nasaha atakayekueleza jinsi ya kukabiliana na hisia zako wakati huu.

You can share this post!

MAPOZI: Kidum

Waandamanaji sasa wapiga kambi katika makao ya wanajeshi

adminleo