• Nairobi
  • Last Updated April 16th, 2024 8:55 AM
President F1: Aina ya nyanya inayostawi maeneo yote nchini Kenya

President F1: Aina ya nyanya inayostawi maeneo yote nchini Kenya

Na SAMMY WAWERU

NYANYA ni mojawapo ya kiungo cha mapishi kinachotumika sana humu nchini, ili kuongeza ladha kwenye mlo.

Hutumika katika kukaanga pamoja na kuandaa kachumbari; mchanganyiko wa nyanya, vitunguu, giligilani, na pilipili hoho (zile kali). Kuna aina mbalimbali ya nyanya, hasa kwa mujibu wa kampuni ama mashirika yanayotafiti na kuuza mbegu.

Kampuni ya kilimo ya Safari Seeds, imetafiti na kuvumbua aina mpya ya nyanya inayohifadhiwa kwa muda wa siku 21. Nyanya zingine huhifadhika kwa muda usiozidi siku saba, yaani wiki moja. Baadhi ya mazao huoza siku tatu pekee baada ya kuvuna.

President F1 

Kulingana na Safari Seeds, kampuni ambayo hushughulikia bidhaa za zaraa, ni kwamba President F1 inastawi katika maeneo ya baridi na joto.

Caroline Njeri, mmoja wa wataalamu wake anasema aina hii ya nyanya ina ustahimilifu wa hali ya juu kwa magonjwa ibuka ya nyanya haswa yanayoshuhudiwa maeneo ya baridi, ikiwamo bakteria.

Bi Caroline Njeri, afisa na mtaalamu wa kilimo Safari Seeds akionesha aina mpya ya nyanya ijulikanayo kama President F1, inayoweza popote pale nchini pamoja na kustahimili magonjwa ibuka ya nyanya. Picha/ Sammy Waweru

“President F1 inastawi maeneo yoyote nchini; yaliyoshamiri baridi na joto. Ingawa haikosi kuathiriwa na magonjwa ya nyanya, ina ustahimilifu wa hali ya juu ikilinganishwa na nyanya zingine,” asisitiza Bi Njeri.

Kulingana na wataalamu wa kilimo ni kuwa nyanya hustawi vyema zaidi katika mazingira ya joto la wastani, kuanzia nyuzijoto 18-27 sentigredi (°C) au 65-75°F.

Meshack Wachira, mtaalamu, anaonya kuwa mvua nyingi husababisha mlipuko wa magonjwa.

“Mvua hujiri na baridi ambayo husababisha magonjwa, kando na kuoza. Kiwango cha joto nacho kinapozidi, mimea hukauka,” aelezea Bw Meshack.

Aidha, zao hili linastawi kwenye aina zote za udongo, kuanzia kichanga, tifutifu na hadi udongo wa kufinyanga. Udongo unastahili kuwa na uchachu wa wastani, yaani pH 6.0-7.0.

Mtaalamu Njeri, anaeleza kwamba President F1 huzalisha nyanya kubwa akikadiria tunda kubwa kuwa na uzito wa karibu gramu 120, hivyo basi ni faida kwa mkulima hususan wanaouza mazao yao kwa kilo. “Ina matunda yenye ngozi ngumu, na yanaweza kusafirishwa masafa marefu bila kuharibika,” anaendelea kusema.

Upanzi

Upanzi wake si tofauti na wa nyanya zingine. Ekari moja inahitaji kipimo cha gramu 50 za mbegu ya President F1, ambacho kinagharimu Sh25,000.

Hata hivyo, Bi Njeri anasema Safari Seeds pia huuza kwa kipimo cha gramu moja, Sh400. “Kwa kawaida ekari moja husitiri karibu mimea 11, 100 ya nyanya. Miche huchukua muda wa kati ya wiki 3-4 kitaluni kuwa tayari kwa uhamishio shambani,” adokeza mdau huyu.

Mtaalamu huyu anapendekeza wakulima kutumia mashimo katika upandaji wa miche. Kipimo cha kutoka shimo moja hadi lingine kiwe futi 2 au sentimita 60. Pia, mstari wa mashimo hadi mwingine uwe na nafasi ya futi 2, Njeri akifafanua kitaalamu kama futi 2 kwa 2.

Urefu wa mashimo kuenda chini, unategemea urefu wa miche na matumizi ya maji. Mkulima, wakati wa upanzi unahimizwa kuchanganya udongo wa juu na mbolea hai au fatalaiza ya kupanda, vizuri.

Mchanganyiko huo, urejeshe shimoni halafu upande miche na unyunyizie maji. Ikumbukwe, miche humwagiliwa maji kabla ya kuing’oa kitaluni, na inaposafirishwa uwe makini. Wakati mwafaka kuipanda ni asubuhi au jioni, makali ya miale ya jua yapunguapo. Jack and the Beanstalk: https://pinupbet.com.ua/jack-and-the-beanstalk

“Ili kuzuia uvukizi wa maji, zingira miche kwa nyasi za boji. Nyasi ni zilizokauka, kwa kuwa hazina wadudu,” ashauri Bi Njeri. Matunzo ya nyanya ni kuzipa maji ya kutosha, palizi, kuzinawirisha kwa fatailaza zifaazo, na kudhibiti magonjwa na wadudu. Mkulima anashauriwa kutumia dawa kwa mujibu wa maelekezo ya mtaalamu.

Wadudu wanaoshuhudiwa sana kwa nyanya ni vithiripi, tuta absolutaspider mites, na leaf miners.

Nyanya huvunwa miezi mitatu baada ya upanzi. Kwa mujibu wa maelezo ya Njeri ni kwamba ekari moja, President F1 ina uwezo wa kuzalisha hadi tani 50. Bei ya nyanya hutegemea msimu na maeneo.

You can share this post!

Jijenge Fund ni mpango mpya wa mkopo unaolenga kunufaisha...

Duka la kwanza la jumla lawapa raha wakazi wa Mandera

adminleo