Habari Mseto

Duka la kwanza la jumla lawapa raha wakazi wa Mandera

April 9th, 2019 Kusoma ni dakika: 2

MANASE OTSIALO

Ilikuwa siku ya furaha kuu mjini Mandera ambapo duka la kwanza la jumla lilifungua malango yake Jumanne asubuhi.

Wenyeji wa mji wa Mandera walijitokeza kwa wingi ili kushuhudia shughuli hio katikati ya mji huo.

Duka la El-Matt lilifunguliwa ili kuwahudumia wakazi hao ambao kwa muda mrefu wamenunua bidhaa kwa maduka ya rejareja.

“Leo nina furaha kubwa sababu duka la jumla limefika Mandera. Aina hii ya maduka yanapatikana Wajir ama Garissa lakini tumeonakaniwa,” alisema mmoja wa wakazi Bi Halima Ahmed.

Bi Ahmed alisema kufunguliwa kwa duka hili kutatoa fursa kwa wenyeji kupata bidhaa eneo moja na vilevile ya ununuzi wa bidhaa utabadilika.

Bw Hussein Ali Haji, Mkurugenzi na mmiliki El- Matt Supermarket alisema amelenga idadi ya binadamu inayozidi kukua kwa kasi mno katika mji wa Mandera.

Duka jipya la El Matt mjini Mandera. Picha/ Manase Otsialo

“Idadi ya watu inaozeka hapa na niliona ni afadhali tuwe na duka la jumla ambamo karibu kila kitu kinapatikana,” alisema.

Bw Haji alisema alitaka sana kushibisha kiu cha wakaazi cha kukosa aina hii ya duka katika kaunti nzima.

Duka hili limejengwa kwa kipande cha ardhi cha urefu wa mita 200 na upana wa mita 100 na askari wa akiba wako hapa kutoa ulinzi kwa wanunuzi.

Hata hivyo ilimgharimu Bw Haji million sabini kwa shughuli nzima ya kujenga na kuweka bidhaa dukani mwake.

“Nimetumia shilingi milioni sabini kufikia hapa na nina imani duka hili litazaa matunda,” alisema.

Bw Haji alisema kujiunga na siasa mwaka wa 2013 ulilemaza ndoto yake lakini alipoondoka katika bunge la kaunti akarejelea shughuli hio.

“Nilikosa nafasi ya kutimiza ndoto yangu nilipokuwa MCA lakini sasa nimefaulu,” alisema.

Hata hivyo tayari watu 21 wameajiriwa hapa na upanuzi wa mradi huu utazidi kutoa nafasi za kazi kwa wenyeji wa Mandera.

“Licha ya kulenga faida, nataka sana kutoa nafasi za kazi kwa wakaazi wa Mandera siku zijaazo,” alisema.

Wateja wa El-Matt supermarket watafurahia huduma kama vile za kufua nguo, sehemu ya kuegesha magari salama na uokaji wa mikate.

Wakulima katika kaunti ya Mandera wamepewa fursa ya kuuza mazao yao kwa duka hili ikiwemo sukuma wiki, maembe, mapapai, machungwa, vitunguu na ndimu.

“Bidhaa zangu zinatoka Mogadishu na Nairobi na nimehakikisha sheria za mipakani zimezingatiwa ninapotoa bidhaa Somalia,” alisema Bw Haji.

Wafanyibiashara wengi wamelalama kufungwa kwa mpaka wa Kenya na Somalia na gharama ya juu kununua bidhaa kutoka Nairobi ikilinganishwa na Mogadishu.

Mmiliki wa duka la jumla la El Matt Bw Hussein Ali Haji aonyesha baadhi ya bidhaa anazouza. Picha/ Manase Otsialo

Safari ya kuenda Mogadishu ni fupi kutokea Mandera kuliko kwenda Nairobi. Mandera kuenda Nairobi ni kilometa 1,200 huku kuenda Mogadishu ikiwa kilometa 500 pekee.

Duka hili litakuwa likifunguliwa saa moja asubui na kufungwa saa mbili usiku lakini katika mwezi mtukufu wa Ramadhani saa za kufunga zitakuwa saa nne unusu usiku.

Wateja 200 wanatarajiwa kuhudumiwa kila siku. “Sijawahi ona duka kama ili maishani mwangu, ni furaha tele kwangu. Nimepata kila kitu nilihitaji hapa ndani. Maajabu haya,” alisema Mzee Haji Hussien, 78.

Mzee Hussien alisema imekuwa kazi ya kuchokesha kutangatanga madukani akitafuta bidhaa.

“Nasema pole kwa watu wa maduka madogo sababu nimehama kuanzia leo,” alisema.

Mwenye duka hili la jumla ameomba serikali ya Kaunti ya Mandera kulegeza sharia za kufanya biashara katika kaunti hii.

Katika mwezi wa Januari, wafanyabiashara walipinga kodi mpya zilizotangazwa na uongozi wa kaunti hii.